ZMBF yashirikiana na IFAD na UNDP kuinua wanawake wakulima wa mwani Zanzibar

1 month ago 17

Bi. Mwinyi ambaye pia ni Mke wa Rais wa Zanzibar alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati wa wiki ya vikao vya ngazi ya juu vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Alikuwa anajibu hoja ya ni kwa jinsi gani ZMBF aliyoiasisi mwaka 2021 imeweza kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs ya Umoja wa Mataifa hususan lile namba 5 la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake.

Amesema ZMBF imeweza kuwafikia wanawake wakulima wa mwani 1,000 kwa hatua mbali mbali. “Kwanza kuwasaidia kuongeza ukulima wao kwa kuwafundisha namna bora ya kulia. Pili kuwapatia mafunzo ya jinsi ya kuendesha biashara zao ndogo ndogo kupitia mwani. Tatu tumeweza pia kuwapatia vifaa, maana elimu iliendana na vifaa.”

Mabadiliko ya tabianchi yachochea vifaa vipya vya kulima mwani

Mwenyekiti huyo wa ZMBF amesema wamewapatia vifaa kama vile boti, mashine za kusagisha mwani.

“Boti zilikuwa muhimu sana kwa kilimo cha mwani kimekuwa kigumu kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Joto likizidi, maji yanakuwa ya moto, kwa hiyo ukulima wa mwani uliokuwa unafanywa katika maeneo karibu na fukwe, inabidi mashamba yaende ndani zaidi. Hivyo boti zinahitajika waweze kufika na wapatiwe mafunzo pia ya kuzamia.”

Wanawake hao pia wamewekwa katika vikundi ili waweze kupatiwa mikopo ya kibiashara.

Jinsi gani wanawake wanaongeza thamani ya mwani?

ZMBF wamechukua hatua mapema baada ya kubaini kuwa mwani uliosagishwa una bei kubwa zaidi kuliko ule unaouzwa kama ulivyo na wanawake Zanzibar.

“Mwani uliokaushwa unauzwa kilo moja shilingi 1,000, chini ya dola moja ya kimarekani. Na ukishasagishwa, kilo moja ya mwani uliosagishwa ni shilingi 10,000 sawa na zaidi ya dola 3.5. Na kama hiyo haitoshi, wanunuzi hao wanaugawa katika vipaketi vidogo.”

Hivyo wamechukua hatua ya kununua mashine na kupatia wanawake mashine za kusagisha mwani badala ya kuuza mwani uliokaushwa.

Halikadhalika pia wamechukua hatua kuboresha mazingira ya ukaushaji kwa kuwapatia vichanja.

“Nia yetu ni kusaka mbinu bora zaidi za kuanika na kusagisha mwani. Tunataka kuja na mpango kamambe wa kutengeneza kiwanda kidogo ambapo mashine tutasimamia wenyewe ZMBF ili tuhakikishe mashine ya kukaushia inafanya kazi. Tutakausha kitaalamu kwa kushirikiana nao,” amesema Bi. Mwinyi.

Programu ya Tumaini ya kuimarisha afya ya wasichana balehe

Hii ni programu ya kutengeneza taulo za kike kwa watoto balehe wa kike ili waweze kwenda shuleni.

“Kuna tatizo kubwa watoto wa kike wanashindwa kwenda shule wakati  wa kipindi cha hedhi. Tumeweza kufikia watoto takribani 5,000 katika shule 36 zilizoko Unguja na Pemba. Hiki kiwanda ni chetu wenyewe, tumekijenga na kuweka vijana wanaoweza kushona.” Unguja na Pemba ni visiwa viwili vinavyounda Zanzibar.

Amesema hilo ndio jambo ambalo anasema ni fahari ya kumwezesha mtoto wa kike katika safari yake ya maisha katika elimu na baadaye ili asichwe nyuma.

Je wanashirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa?

Bila shaka, tuna ushirikiano mzuri, amesema Bi. Mwinyi akitaja Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, IFAD ambao walisaidia mafunzo ya kilimo bora cha mwani na kuwapatia vifaa. Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP lilisaidia elimu ya biashara kwa wanawake wakulima wa mwani.

Source : UN Habari

SHARE THIS POST