Zanzibar ni salama kwa utalii wa mikutano na makongamano ya Kimataifa

2 months ago 297

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar ni nchi salama kwa utalii wa mikutano na makongamano ya kimataifa.

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 12 Oktoba 2024, kwenye Kongamano la Kwanza la Kiislamu la Kimataifa lililowakutanisha Mashehe mbalimbali kutoka mataifa 18 duniani, kwenye viwanja vya “New Amani Complex,” Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema Zanzibar ina fursa kubwa ya kukuza utalii wa maadili, “Halal Tourism,” kama chanzo cha mapato na ajira kwa watu wake. Kupitia kongamano hilo la Kiislamu la kimataifa, limetoa mwangaza kwa nchi kama sehemu ya utalii wa maadili, hasa kwa wageni wanaokuja kuitembelea, si tu kujifunza dini lakini pia kufurahia uzuri wa mandhari, haiba ya nchi, mila, silka, utamaduni, na ukarimu wa watu wake.

Halikadhalika, Alhaj Dk. Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa mikusanyiko kama hiyo na kuunga mkono jitihada za taasisi binafsi na za serikali, ikiwemo kukuza uchumi na maadili ya nchi ili kupatikane jamii yenye maadili, na kuiweka nchi kwenye hadhi ya utalii wa maadili ambao hivi sasa umeshika kasi duniani.

Naye, Mufti Ismael Menk kutoka nchini uingereza, ambaye ni mmoja wa watoa mada wakuu katika kongamano hilo, amesema maendeleo ya taifa lolote duniani hayatimii pasi na kuwepo kwa ustawi wa amani na usalama kwa nchi na watu wake, kwa kuendeleza na kudumisha umoja, upendo, na kuheshimiana miongoni mwa jamii.

 

 

 

 

 

 

Source : Millardayo.com

SHARE THIS POST