Elisabeth alikuwa msichana mdogo alipobakwa na mwanamume.

10 Oktoba 2024 Haki za binadamu

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema zaidi ya wasichana na wanawake milioni 370 walioko hali hii leo, walikumbwa na ukatili wa kingono wakati wa utoto wao, yaani kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Makadirio ya kwanza kabisa ya kimataifa na kikanda kuhusu ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto ambayo yamechapishwa mkesha wa  Siku ya Kimataifa ya Msichana yanaonesha ukubwa wa ukiukwaji huu duniani kote, hasa kwa wasichana balehe, ambao mara nyingi huwa na athari za kudumu.

Akizungumza leo katika mkutano wa waandishi wa habari huko New York, Marekani, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) Catherine Russell amesema, "ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto ni doa kwenye dhamiri yetu ya maadili. Unaleta majeraha makubwa na ya kudumu, mara nyingi ukitendwa na mtu anayejulikana na kuaminiwa na mtoto, katika maeneo ambapo mtoto huyo  anapaswa kujihisi salama."

Kulingana na ripoti hii, kwa kujumuisha aina za ukatili wa kijinsia zisizo na mawasiliano ya moja kwa moja, kama vile unyanyasaji mtandaoni au wa maneno, idadi ya wasichana na wanawake walioathiriwa inafikia milioni 650 duniani kote au mmoja kati ya 5, ikisisitiza umuhimu wa dharura wa mikakati kamili ya aina zote za ukatili na unyanyasaji.

“Watoto katika mazingira dhaifu wako katika hatari kubwa zaidi ya ukatili wa kijinsia,” amesema Russell. “Tunaona ukatili wa kijinsia wa kutisha katika maeneo ya migogoro, ambapo ubakaji na ukatili wa kijinsia mara nyingi vinatumiwa kama silaha za vita.”

Ripoti hiyo pia imebaini kwamba ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto umeenea, ukikata mipaka ya kijiografia, kitamaduni, na kiuchumi. Kulingana na takwimu Afrika ya Kusini mwa Sahara ina idadi kubwa zaidi ya waathirika. Aidha, ripoti hiyo inafafanua kwamba wasichana katika mazingira dhaifu kama vile yale yenye taasisi dhaifu, vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, au idadi kubwa ya wakimbizi wanaokimbia kutokana na mizozo ya kisiasa au usalama, wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu, ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto hutokea zaidi wakati wa balehe, huku kukiwa na ongezeko kubwa kati ya umri wa miaka 14 na 17. Utafiti unaonesha kwamba watoto wanaopitia ukatili wa kijinsia wana uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na unyanyasaji wa mara kwa mara.

Ripoti hio imebaini kwamba, waathirika mara nyingi hubeba jeraha la ukatili wa kijinsia hadi utu uzima, wakikabiliwa na hatari kubwa ya magonjwa ya zinaa, matumizi mabaya ya dawa, kutengwa kijamii, na matatizo ya afya ya akili kama vile wasiwasi na unyogovu, pamoja na changamoto katika kuunda mahusiano yenye afya. Na kwa mujibu wa tafiti athari hizo zinaongezeka zaidi wakati watoto wanachelewesha kufichua matukio ya unyanyasaji huo, mara nyingine kwa vipindi virefu, au wanaposhikilia siri ya unyanyasaji kabisa.

Takwimu pia zinaonesha kwamba ingawa wasichana na wanawake wengi zaidi wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia na matukio yao kunakiliwa vizuri, wavulana na wanaume pia wanaathirika. Upungufu wa takwimu unaodumu, hasa kuhusu matukio dhdi ya wavulana na aina za ukatili wa kijinsia zisizo na mawasiliano ya moja kwa moja, unaashiria umuhimu wa kuongezauwekezaji katika ukusanyaji wa takwimu ili kupata picha kamili ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.

Wakati viongozi wa serikali, wanaharakati, waathirika, na vijana wanapojipanga kwa ajili ya Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Mawaziri kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto nchini Colombia mwezi ujao, takwimu za hivi karibuni zinaonesha umuhimu wa dharura wa hatua za kimataifa dhidi ya ukatili wa kijinsia katika utotoni.

Kipaumbele kikuu ni pamoja na kubadilisha mitazamo na tamaduni zenye madhara, kuwapa watoto taarifa sahihi na zinazopatikana kwa urahisi, kuhakikisha waathirika wanapata haki na huduma za kuponya, kuimarisha sheria za kuwakinga watoto, na kuwekeza katika rasilimali za utekelezaji. Aidha, kuboreshwa kwa mifumo ya kitaifa ya takwimu ni muhimu ili kufuatilia maendeleo na kudumisha uwajibikaji kwa kutumia viwango vya kimataifa.