Wizara yaja na mpango kukomesha uvuvi haramu

3 months ago 20

Unguja. Ili kukomesha uvuvi haramu unaotajwa kushamiri kwa kutumia nyavu ndogo, Serikali imebuni mpango mkakati wa kutengeneza boti kubwa za uvuvi na kuwapatia wananchi.

Hayo yamebainishwa Julai 26, 2024 na  Waziri wa Uchumi wa Buluu, Shaaban Ali Othman katika mkutano wa pamoja kati ya viongozi wa wizara hiyo, kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kusini Unguja, wananchi na wavuvi wa ukanda wa ghuba ya Chwaka, wakati wa kusikiliza changamoto za wavuvi na kuzipatia suluhu.

“Wizara imeamua kuja na ufumbuzi kwa kutengeneza boti kubwa za uvuvi zenye urefu wa mita nane na uwezo wa kufika kina kirefu cha maji kwa ajili ya ukanda wa kusini, hususan ghuba ya Chwaka ili eneo lililotengwa kwa ajili ya uhifadhi liendelee kuzalisha samaki wengi zaidi,” amesema.

Mbali na kutengeneza boti hizo, pia Serikali itasimamia utoaji nyavu zinazoruhusiwa kutumika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Hata hivyo, Shaaban amesema mbali na mapendekezo hayo waliyoyatoa, Wizara ipo tayari kusikiliza maoni ya wavuvi na kuyafanyia kazi.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub  Mohammed Mahamoud amesema suala la kukimbizana kati ya wavuvi na wasimamizi wa eneo la hifadhi la samaki si jambo zuri kwani linahatarisha usalama wao, hivyo ni vyema wavuvi kukubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na Serikali ili upatikane ufumbuzi wa haraka.

Baadhi ya wavuvi wamesema iwapo watapatiwa nyenzo muhimu zitawasaidia kuachana na uvuvi huo, kwani changamoto kubwa hawana vifaa vya kwenda kina kirefu cha maji.

Wamesema wameyapokea mapendekezo hayo yaliyotolewa na Serikali wakiomba Wizara ya Uchumi wa Buluu kupitia wataalamu wake kuendelea kufanya uchunguzi wa kina juu ya matumizi ya bahari kwa ukanda wa ghuba ya Chwaka.

“Siyo kwamba wavuvi wanapenda kuvua kiharamu kila mmoja angetamani kuona anavua samaki wazuri na kuongeza kipato lakini kwa sababu ya kukosa nyenzo, ndiyo maana wengi wanazungukia katika maeneo ya karibu ambayo ni hifadhi kwa hiyo tunapongeza mpango huu utasaidia,” amesema Haji Suleiman Issa.

Source : Mwananchi

SHARE THIS POST