WAZIRI NDEJEMBI ATAKA UADILIFU NA KUTENDA HAKI KWA WATUMISHI WA SEKTA YA ARDHI

3 months ago 20

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuongeza uadilifu na kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yao sambamba na kuongeza kasi katika utendaji kazi.

Mhe. Ndejembi namesema, suala la ardhi ni gumu na linahitaji watumishi kuwa makini ambapo amesisitiza kuwa ni lazima watumishi wa sekta ya ardhi watende haki huku wakizingatia kuwa kuna sheria, kanuni na miongozo inayowaoongoza katika utendaji kazi.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema, yale yote mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake ikiwemo Klinik za Ardhi atayaendendeleza kwa lengo la kuleta ufanisi wa wizara.

‘’Sikuja kutengua torati, yote aliyoyaanzisha mtanguluzi wangu ikiwemo klinik za ardhi zitaendelea na vile vile anayehisi jambo lake limekwama ajitokeze na atahudumiwa’’ amesema Mhe. Ndejembi.

Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo tarehe 26 Julai 2024 wakati akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa Wizara ya Ardhi mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kutoka kuapishwa kushika nafasi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake Mhe. Jerry Silaa.

Sambamba na hayo Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametaka kuimarishwa kwa mifumo ndani ya wizara ili migogoro ya ardhi isiendelee kujitokeza.

Mhe. Ndejembi ameapishwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akitokea Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu).

 

Source : Millardayo.com

SHARE THIS POST