Mvua kubwa ilisababisha maporomoko ya udongp katika kijiji kilichoko juu ya mlima katika eneo la mbali la Gofa nchini Ethiopia.
25 Julai 2024 Msaada wa Kibinadamu
Idadi ya watu waliokufa baada ya matukio matatu ya maporomoko ya udongo kusini mwa taifa hilo yaliyochochewa na mvua kubwa imeongezeka na kufikia 257 jana Jumatano huku idadi ikitarajiwa kufikia 500, na kwamba watu zaidi ya 15,000 wanatakiwa kuhamishwa.
Imesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA. Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na kutuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na serikali ya Ethiopia, amesema Umoja wa Mataifa unashirikiana na serikali na wadau kutathmini kiwango cha uharibifu na hatua za usaidizi.
Serikali ya Ethiopia hivi sasa inakamilisha mpango wa kuwahamisha waathirika wa maporomoko hayo ya udongo.
Kwa mujibu wa OCHA Timu za mashirika ya kutathmini misaada ya kibinadamu ilifika eneo hilo na kwa sasa inaunga mkono uratibu wa hatua za msaada kupitia kituo cha uratibu wa dharura nchini humo.
Msaada unaendelea kutolewa
Shirika la Msalaba Mwekundu la Ethiopia limewasili katika eneo hilo leo, tangu juzi tarehe 23 Julai, likiwa na malori nne yenye vifaa vya kuokoa maisha.
Ofisi ya afya ya jimbo lililoathirika imepeleka magari mawili na vifaa tiba katika eneo la tukio na inajiandaa kutuma timu ya wataalam wa afya.
Mashirika ya misaada yanatenga rasilimali za kifedha na za aina nyingine kwa ajili ya kukabiliana na dharura hiyo ambayo pia mbali ya kukatili maisha ya watu imesababisha uharibifu Mkubwa wa mioundombinu lakini sambazaji wa vifaa unaendelea katika sekta zote.