11 Oktoba 2024 Haki za binadamu
Vitendo vya unyanyasaji na unyonyaji wa kingono dhidi ya watoto vimeongezeka katika mazingira ya kidijitali, huku zaidi ya watoto milioni 300 kwa mwaka wakikadiriwa kuwa waathiriwa wa vitendo hivyo mtandaoni, anasema Mama Fatima Singhateh ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na unyanyasaji wa kingono wa watoto.
Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, Mtaalamu huyo wa haki za binadamu ananukuliwa kutoka katika ripoti aliyoiwasilisha kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, "teknolojia inatoa mianya mingi ya fursa za kulinda na kudumisha haki za watoto, lakini uwezo wake wa haraka, unaobadilika na ambao haujawahi kushuhudiwa unaleta hatari kubwa kwa watoto na kuwaweka kwenye madhara."
Ripoti hiyo inafafanua jinsi matumizi mabaya ya teknolojia zilizopo na zinazoibukia yanavyozidisha hali ya watoto kukutana na hatari, madhara na aina mbalimbali za unyanyasaji na unyonyaji wa kingono.
"Teknolojia zilizopo zinatumika vibaya kunyanyasa kingono, kuchukua na kusambaza picha na video bila ridhaa, kuzalisha maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto, kuwalawiti watoto na kupeperusha mbashara mitandaoni unyanyasaji wa kingono wa watoto," Singhateh anasema.
"Teknolojia zinazoibuka kama vile video bandia, kubadilisha video kuwa za ngono, kupunguza kuzeeka, akili mnemba, usambazaji wa mafaili kati ya watu wa rika moja na pia teknolojia ya kutumia sauti ya mtu mwingine kwa mtu mwingine, vinaongeza nji zilizopo za kunyonya watoto na kutengeneza nyenzo za unyanyasaji wa kingono kwa watoto," mtaalam huyo aanasisitiza.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa bila hatua za haraka, jambo hilo litachochewa zaidi na ukosefu wa usawa uliokuwepo hapo awali, na kusababisha ukiukwaji wa ziada wa haki za watoto, na athari zisizo sawa kwa wale wanaotoka katika makundi yaliyo hatarini na yaliyo pembezoni.
Mtaalamu huyo huru wa Umoja wa Mataifa anasema, "Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali uliopitishwa hivi majuzi unaimarisha dhamira yetu ya kimataifa ya kufanya nafasi ya mtandaoni kuwa salama kwa wote, hasa kwa watoto, kupitia hatua za serikali, makampuni ya teknolojia na mitandao ya kijamii.”
"Serikali lazima ziimarishe mifumo ya kisheria inayowaadhibu wale wanaotumia vibaya mazingira ya kidijitali kuunda, kusambaza maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto, na kuanzisha utaratibu mzuri wa kitaifa wa kutekeleza uangalizi wa udhibiti," Singhateh anasema.
"Kampuni za teknolojia lazima ziwekeze katika uthibitishaji wa umri, udhibiti wa maudhui yanayofaa watoto, na njia za rufaa na huduma za usaidizi. Uzingatiaji wa Kanuni Elekezi za Biashara na Haki za Kibinadamu lazima iwe kipaumbele kwa kampuni hizi.
Mama Singhateh anahimiza wadau wote kuhakikisha ushiriki wa mtoto katika michakato ya kufanya uamuzi na kuweka viwango vya kiufundi.