Wataalamu wafanikiwa kukuza meno ya binadamu katika maabara

Ingawa viumbe wengi wana uwezo wa kukuza upya meno yao kwa zaidi ya mara moja, wanadamu hupata nafasi ya kukuza meno mapya mara moja tu wakati wa kukamilisha seti nzima ya meno.
Wanasayansi kutoka Chuo cha King's College London, Uingereza wamefanikiwa kukuza jino la binadamu kupitia maabara.
Ingawa mafanikio haya bado yanaweza kuwa na safari ndefu hadi kufikia kuziba mapengo katika kinywa cha mtu, watafiti wanasema ni hatua kubwa katika utafiti.
"Wazo la kulikuza tena jino kwa njia ya kibaolojia, linavutia," anaeleza mtaalamu wa meno, Dk Ana Angelova-Volponi. "Kwa kukuza jino tena, tunajaza mapengo."
Tabasamu la ukiwa na meno kamili linatafutwa sana. Watu wengi hugeukia meno ya bandia au kupandikiza ili kuwapa mwonekano mzuri. Lakini meno ya kupandikiza yanaweza kusababisha matatizo yasiyotarajiwa.
"Meno ya kupandikiza yanahitaji upasuaji na uwekaji mzuri wa meno hayo katika mfupa," anaeleza Xuechen Zhang, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa PhD katika Kitivo cha Meno na Kinywa.
"Meno yaliyokuzwa maabara yanaweza kukua upya, kuunganishwa kwenye taya kama meno halisi.
"Yatakuwa na nguvu zaidi, ya kudumu, na yasiyo na hatari, ni suluhisho la kudumu zaidi na linaloendana na bayolojia kuliko kujazwa meno ya kupandikiza.
Mchakato wa kukuza

Timu ya utafiti, kwa ushirikiano na Chuo cha Imperial London, wamefaulu kuanzisha aina maalumu kifaa ambacho kinawezesha seli kuwasiliana na seli nyingine.
Hii ina maana seli moja inaweza kuiambia seli nyingine ianze kuwa seli ya jino, na inaiga mazingira ya kukua kwa meno na kuruhusu wanasayansi kuunda upya mchakato wa maendeleo ya meno katika maabara.
Baada ya kufanikiwa kuunda mazingira yanayohitajika kukuza meno, wanasayansi sasa wanahitaji kufikiria jinsi ya kuyatoa maarifa hayo kutoka katika maabara hadi kwenye mdomo wa mtu. Na hilo linaweza kuchukua miaka mingi.
Kuna mawazo kadhaa; tunaweza kupandikiza chembechembe changa za meno mahali penye pengo na kuziacha zikue ndani ya mdomo," anasema Zhang.
"Au tunaweza kuunda jino zima kwenye maabara kabla ya kuliweka kwenye mdomo wa mtu."
Lakini njia yoyote ambayo wanasayansi watachagua, mchakato wa awali huanza kwenye maabara.
Athari ya meno mabovu

Afya duni ya kinywa inaweza kuathiri uwezo wa watu wa kula, kuzungumza na kujumuika na wengine, na inahusishwa na matatizo ya moyo na maambukizi iwapo bakteria wataingia kwenye mkondo wa damu. Wazee wako hatarini zaidi.
Zaidi ya nusu ya watu wazima ambao wanaishi katika nyumba za wazee wana meno yaliyooza, ikilinganishwa na 40% ambao hawaishi katika nyumba za utunzaji, kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Ubora na Utunzaji wa Jamii.
Saoirse O'Toole, mhadhiri wa magonjwa ya viungo vya uzazi katika Chuo cha King's College, anasema: "Teknolojia hii mpya ya kukuza meno inasisimua sana na inaweza kubadilisha taaluma ya madaktari wa meno.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi