WANAJESHI NANE WA ISRAEL WAUAWA, “Waliingia katika mtego wa Hezbollah”

1 month ago 20


Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema askari wake nane wamefariki katika shambulio wakati wa operesheni ya ardhini inayoendelea eneo la Kusini mwa Lebanon. Taarifa ya wanajeshi hao kuuawa imethibitishwa na IDF leo Jumatano Oktoba 2,2024, ambapo wanajeshi hao wanatajwa kuwa waliingia katika mtego wa wanamgambo wa Hezbollah kisha kumiminiwa risasi zilizopelekea vifo vyao. Mauaji ya wanajeshi hao yametokea ikiwa ni siku moja tangu Iran irushe makombora zaidi ya 200 kwenda nchini Israel. Hata hivyo makombora hayo yalidhibitiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo wa kujilinda wa Israel maarufu kama Iron Dome. Kwa mujibu wa IDF wanajeshi hao wameuawa katika jitihada za kuungana na wenzao ambao wanaendelea na operesheni ya ardhini huko Kusini mwa Lebanon, eneo ambalo linatajwa kukaliwa na Hezbollah. Huenda operesheni na uvamizi wa Israel nchini Lebanon ukawawia ugumu kutokana na namna wanamgambo hao wa Hezbollah wanavyojibu mapigo tofauti na ilivyofanyika dhidi ya kundi la Hamas lenye makao yake eneo la Gaza nchini Palestina. Helkopta ya Israel imeonekana ikitua eneo yalipotokea mauaji hayo na kuchukua miili ya wanajeshi hao kuwarejesha katika taifa lao kwa ajili ya mazishi. Mzozo baina ya pande hizo, ambao sasa umesambaa na kuihusisha Iran tayari umeanza kuleta madhara ambapo tayari kumeanza kuripotiwa ongezeko la bei ya mafuta kwa dumu. Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), bei ya mafuta ya Marekani imepanda kwa asilimia 3 na kufikia zaidi ya Dola 70 za Marekani(Sh190,750) kwa pipa, huku mafuta ghafi aina ya Brent yakiuzwa kwa Dola 73 za Marekanio (Sh 198,925) kwa pipa. Mwaka uliopita, masoko ya nishati yalionesha utulivu licha ya mvutano unaoongezeka Mashariki ya Kati, baada ya Houthi ambalo ni kundi la kiislamu na kisiasa lililoanzia Yemen miaka 1990, kuweka marufuku dhidi ya meli za mizigo kwenye Bahari Nyekundu. Hofu kuu imekuwa juu ya kuzorota kwa hali inayoweza kusababisha Tehran kufunga mlango wa Hormuz, njia muhimu ya kusafirisha mafuta ghafi kutoka Ghuba. Hofu hii sasa inaathiri masoko, wakati ambao benki za dunia zilikuwa zikitangaza kuwa mshtuko wa mfumuko wa bei wa miaka mitatu iliyopita ulikuwa umepungua. BBC inaeleza kuwepo kwa hali ya wasiwasi kwamba sasa Ulaya inategemea sio tu mafuta bali pia LNG (gesi ya kimiminika inayosafirishwa ikiwa imegandishwa) kutoka Qatar, ambayo pia hupita kwenye mlango wa Hormuz, ambao ni mwembamba hadi maili 20. Hayo yanakuja wakati tayari vita vya Russia na Ukraine vikisababisha nchi za Ulaya kutegemea soko la kimataifa la LNG. Inaelezwa kuwa, licha ya bei za mauta kuwa bado chini ikilinganishwa na mapema mwaka huu, mzozo wa kijiografia wa wakati mmoja unafufua kumbukumbu za enzi za mfumuko wa bei za miaka ya 1970. Jana Jumanne, Oktoba 1, 2024 Ikulu ya Marekani ilitangaza inaamini Iran inajiandaa kwa shambulizi la kombora la masafa marefu dhidi ya Israel na ghafla bei ya pipa la mafuta ghafi imepanda kwa kasi kwenye masoko ya kimataifa baada ya taarifa hiyo. Ukiachilia mbali ongezeko la mafuta hayo, Israel imempiga marufuku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuingia nchini humo huku kitendo cha UN kutolaani mashambulizi ya makombora ya Iran nchini Israel kikitajwa kuwa sababu. Hadi sasa bado Antonio Guterres hajasema chochote kuhusiana na uamuzi huo wa Israel wa kumuwekea zuio la kuingia nchini Israel. Mkuu wa majeshi ya Israel Luteni Jenerali Herzi Halevi, Mkuu wa Shirika la Ujasusi wa Ndani la Shin Bet Jasusi, Ronen Bar na Mkuu wa Shirika la Ujasusi wa nje la Mossad, Jasusi David "Dadi" Barnea wamekutana asubuhi ya leo katika kikao cha kutathimini hali ya mambo baada ya mashambulizi ya Iran jana yenye lengo la kulipiza kisasi cha mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Hanie na kiongozi wa Hezbola Hasaan Nasrallah. Video na MGONGO KAITIRA.
Source : Mwananchi Digital

SHARE THIS POST