Walio 'single' watajwa kuwa hatarini kupata tatizo la afya ya akili, Wataalamu wataja kinachotokea
Wakati baadhi ya vijana wakidai kutokuwa kwenye mahusiano (single) wanafurahia, mtaalamu wa afya ya akili amedai wapo hatarini kupata tatizo la afya ya akili. Kauli hiyo inakuja katika kipindi ambacho imebaki siku chache kuadhimisha Siku ya Afya ya Akili Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Oktoba 10. Akizungumza na Mwananchi Digital Daktari Bingwa wa Afya ya Akili Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC), Matiko Mwita bila kutaja takwimu amedai tafiti zinaonyesha kuwa mtu asiyekuwa na mahusiano ni rahisi kupata msongo wa mawazo kuliko yule aliyeko kwenye mahusiano kwani anakuwa hana mtu wa kumweleza shida zake. Hata hivyo, nao baadhi ya vijana jijini Mwanza wakizungumza na Mwananchi Digital wamekuwa na maoni mseto kuhusiana na hilo huku baadhi yao wakiunga mkono na wengine wakidai kuwa single inapunguza msongo wa mawazo unaosababishwa na wenza wao.