Wakulima wa viazi lishe mkoani Singida Tanzania walionufaika na mafunzo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kiliimo, FAO.
24 Julai 2024 Ukuaji wa Kiuchumi
Faida kubwa ya viazi lishe ni kwamba ina kiasi kikubwa cha Vitamini A na hivi viazi lishe vimetusaidia sana kwenye lishe majumbani na vile vile kiuchumi kwa kuwa ninauza mbegu, anasema Michael Aloyce, mkulima kutoka wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, katikati mwa Tanzania ambaye amenufaika na mafunzo yaliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO.
Akizungumza akiwa kwenye shamba lake la ukubwa wa eka moja, Bwana Aloyce anajinasibu kufahamu aina mbalimbali za viazi lishe akitaja kuwa ni pamoja na Mataya, Kiegeya, Kakamega na Nasputi. Anasema ufahamu wote wa virutubisho ndani ya viazi hivyo pamoja na aina yake unatokana na mafunzo waliyopatiwa na FAO na washirika wake.
Mradi unatekelezwa Singida, Zanzibar na Dodoma
FAO Tanzania inasema hivi sasa inatekeleza mradi wa pamoja wa kuongeza kasi ya uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake vijijini, mradi unaotekelezwa kwenye wilaya hiyo ya Ikungi,singida pamoja na wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na huko Zanzibar kwenye wilaya za Kati na Kusini mkoa wa Kusini.
Wanaume kama Bwana Aloyce wamejumuishwa kwenye mradi huo ambapo wako asilimia 15. Lengo ni kuona wanasaidiana kuzalisha mazao shambani na wake zao waliochaguliwa kwenye mradi huu.
Elimu imetuongezea ujuzi na kipato
Bwana Aloyce anasema “nawashukuru sana FAO na wataalamu wetu kwa kuendelea kutuhumidia sisi wakulima na kupata elimu ambayo itatuwezesha pia kuongeza kipato kwenye maisha yetu na hasa kuondokana na udumavu hasa wa akili kwa watoto wetu.”
Ameenda mbali kushauri wakulima wenzake waendelee kulima viazi lishe.
Mwanzoni mwa mradi, wakulima walikuwa hawana hamasa ya kilimo cha viazi lishe, na vile vile suala la mbegu za viazi hivyo lilikuwa ni changamoto, amesema Mkuu wa Idara ya Kilimo wilaya ya Ikungi, Gurisha Msemo.
Wakulima pia wanapanda mbegu na kusambaza kwa wenzao
Walichagua wakulima 12 akiwemo Bwana Aloyce ili washiriki pia katika kuzalisha mbegu za viazi lishe.
“Kwa mfano hivi sasa, Afisa kilimo wa wilaya ameshaandaa utaratibu wa kusambaza kwa wakulima wengine mbegu kupitia kwangu. Amenunua mbegu kwangu na kuzisambaza,” anasema Bwana Aloyce akishukuru wataalamu wa kata, wilaya na FAO.
“Ninashauri wakulima wenzangu tuendelee kulima viazi lishe,” anasema Bwana Aloyce ambaye pia shamba lake pia ni la mbegu za viazi hivyo.
Akitamatisha Afisa kilimo anaelezea faida ya viazi lishe akisema wakulima kwanza wanapata lishe nyumbani, mathalani kupitia baadhi ya viazi ambavyo majani yake ni mboga au matembele. Halikadhalika amesema viazi lishe vimesaidia pia wakulima kuongeza vipato vyao kwani viazi hivi vina bei zaidi kuliko viazi vingine vya kawaida.