Wafahamu wabakaji watano hatari zaidi kuwahi kutokea duniani - BBC News Swahili

2 days ago 55

Wafahamu wabakaji watano hatari zaidi kuwahi kutokea duniani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika kipindi cha juma moja lililopita, dunia imeshuhudia taarifa nyingi za ubakaji nyingi zikitokea Ulaya. Muigizaji maarufu na mchekeshaji Russell Brand nchini Uingereza amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ubakaji zilizotokea kati ya mwaka 1999 na 2005, na atapanda kizimbani tarehe 2 Mei.

Vilevile, babu mwenye umri wa miaka 78, Alan Vinten, amehukumiwa kifungo cha miaka 17 jela kwa kumbaka mara kadhaa mtoto wa miaka 9 karibu miaka 50 iliyopita, enzi za miaka ya 1970. Hukumu kama hiyo pia imetolewa kwa mbakaji mwingine, Jeffrey Rose, mwenye umri wa miaka 75, ambaye amekutwa na makosa 20 ya ubakaji na unyanyasaji kingono yaliyotokea miaka 40 iliyopita.

Aidha, Juma lililopita mwanafunzi wa China, Zhenhao Zou, amekutwa na hatia ya kubaka wanawake 10 kwa kuwawekea dawa za kupoteza fahamu, huku wengine 23 wakijitokeza zaidi katika kesi inayotikisa Uingereza na Ulaya kwa sasa.

Mahakama ya ndani ya London ilielezwa mwezi uliopita kuwa, Zou alikuwa akiwalaghai wanawake kupitia hila mbalimbali kabla ya kuwanyanyasa kingono.

Wapelelezi wanakadiria kuwa zaidi ya wanawake wengine 50 duniani kote huenda walibakwa na kunyanyaswa kingono na mwanafunzi huyo wa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London.

Kesi yake imevuta hisia kali ulimwenguni, huku wengi wakitaka ahukumiwe kwa ukali zaidi.

Lakini katika historia ya uhalifu wa ngono, kuna wahalifu waliovuka viwango vya kawaida kwa kuwa na idadi kubwa ya waathirika ama watu waliowabaka. Ingawa wapo wengine kesi zikiendelea, lakini hawa ni baadhi ya wabakaji waliofanya uhalifu wa kutisha zaidi duniani na kuhukumiwa kifungo.

1. Reynhard Sinaga (Uingereza)

.

Chanzo cha picha, Greater Manchester Police

Huyu ni mbakaji mwenye rekodi mbaya zaidi katika historia ya Uingereza. Yeye hakuwa anabaka wanawake, bali aliwalenga wanaume. Na alitumia njia ya kuwapa dawa za kupoteza fahamu na kutumia mwanya huo kuwanyanyasa kingono na kuwaingilia.

Sinaga alifungwa maisha mwaka 2020 baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kulevya na kuwabaka wanaume 48 katika nyumba yake ya kifahari mjini Manchester.

Polisi wanaamini kuwa mwanafunzi huyo alihusika kuwalenga zaidi ya wanaume 200.

Daniel, mwathirika wa kwanza kuamua kueleza kkilichomkuta, aliiambia BBC wakati huo kuwa "sikuweza kukumbuka chochote" alipozinduka katika gorofa ya Sinaga.

Ni wakati tu wapelelezi wa Greater Manchester Police walipomwonyesha picha za shambulio hilo miaka miwili baadaye ndipo alipogundua kuwa alikuwa amebakwa. Kwa miaka miwili hakujua.

"Inasikitisha kujiona ukiwa hatarini kwenye picha (za video) ambazo mtu mwingine amepiga," alisema.

"Unaweza kuona ... naonekana kupoteza fahamu kabisa."

Sinaga, raia huyu wa Indonesia anatumikia kifungo kisichopungua miaka 40 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa 159 ya ngono mnamo Januari 2020. Ingawa inasadikiwa idadi halisi inaweza kufikia 206. Alikuwa akiwalaghai wanaume waliokuwa wamelewa, akiwaongezea dawa za kulevya na kuwabaka akiwa pia amewapiga picha za video. Alitenda vitendo hivyo kati ya mwaka 2005 mpaka 2017.

2. João Teixeira de Faria "John of God" (Brazil)

.

Chanzo cha picha, AFP

Alijulikana kama mganga wa kiroho lakini aligeuka kuwa mbakaji wa mamia ya wanawake. Baada ya miaka mingi ya shutuma, zaidi ya wanawake 600 walijitokeza kumshutumu kwa unyanyasaji wa kingono.

Mwanamke mmoja aliyetoa ushahidi wake mwenye umri wa miaka 39 aliwaambia polisi kwamba mnamo Oktoba 24, 2018, Faria, 76, alimkaribisha ofisini kwake kwa kikao cha faragha katika kituo cha uponyaji cha Casa de Dom Inacio de Loyola katika mji wa Abadiânia. Anasema walipokuwa ndani ya ofisi yake, alizima taa na kumfanyia unyanyasaji huo, kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka iliyokuwa inaendesha kesi ya mbakaji huyo.

"Waathiriwa walienda kutafuta tiba. [John of God] alichukua fursa ya hali hiyo kwa kuwnyanyasa kingono," alisema Valdemir Pereira, mkuu wa polisi wa Jimbo la Goiás.

Alifungwa miaka 19 gerezani kwa makosa ya unyanyasaji wa kingono na ubakaji.

3. Billy Joe Godfrey (Marekani)

Mtu huyu alikutwa na hatia ya kuwatesa kingono, kuwabaka na kuwaua wavulana 142. Alikiri mauaji 221, na ubakaji wa watoto wengine zaidi ya 200+. Na baada ya hayo yote, alikaribia kuachiliwa baada ya kutumikia kifungo cha miaka 22 tu.

Alitenda makosa haya kwa miongo kadhaa akitumia nafasi yake kama mtu wa jamii kuwadanganya watoto na vijana wadogo kabla ya kuwadhulumu. Alifungwa kifungo cha maisha gerezani.

4. Luis Garavito (Colombia)

.

Chanzo cha picha, Poveda

Anajulikana kama "The Beast" kwa sababu ya unyama wake. Garavito alihukumiwa kwa kumbaka, kuwatesa, na kuwaua zaidi ya 138 watoto wa kiume, ingawa idadi halisi inakadiriwa kuwa zaidi ya 200. Watoto hao walikuwa na umri kati ya miaka 6 mpaka 16. Kutokana na umri wa watoto hawa, Garavito alisababisha hisia kubwa za chuki na simanz kwa familia za waathirika na jamii kwa ujumla. Hii inamfanya kuwa mmoja wa wabakaji wa watoto wakubwa zaidi katika historia duniani.

Watu hawa walitenda uhalifu wa kutisha, wakiacha alama za maumivu kwa waathirika wao. Kupitia mifano yao, jamii inapaswa kuwa makini na kuongeza juhudi za kuzuia na kupambana na unyanyasaji wa kingono ili kulinda watu wote, hasa wanawake na watoto, dhidi ya wahalifu wa aina hii.

5. Richard Allen Minsky (Marekani)

Anajulikana kama "The Con Artist Rapist". Mbakaji aliyebaka wanawake kwa takriban miongo miwili katika majimbo kadhaa nchini Marekani. Minsky angewalaghai wanawake kuwabaka na kuwafanyia ukatili mwingi wa kingono. Alitajwa kubaka wanawake zaidi ya 100 kwa nyakati tofauti. Minsky alikuwa akiingia na kutoka gerezani kwa makosa machache ya mara kwa mara ambayo alikuwa akikutwa naayo, kabla ya kukamatwa tena kwa makosa ya ubakaji ya wanawake karibu kila kona ya Marekani. Mpelelezi wa LAPD John Metcalf, ambaye alipewa kazi ya kumfuatilia Minsky, aliweka wazi namna ilivyokuwa muhimu jamii kusaidia kumtia mikononi na baadaye hatiani. Jaji aliyetoa hukumu alisema kuwa wahalifu wa ajabu duniani kama Minsky walikuwa adimu. Alihukumiwa kifungo cha maisha jela na bado yuko jela mpaka sasa.

Source : BBC Swahili

SHARE THIS POST