Walinda amani wa UNIFIL wakipiga doria katika eneo la Tiro, kusini mwa. (Maktaba) Lebanon

10 Oktoba 2024 Amani na Usalama

Nchini Lebanon ujumbe wa jeshi la Umoja wa Mataifa la mpito nchini humo, UNIFIL, unasema mapigano kati ya jeshi la Israeli, IDF, na wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Lebanon yamekuwa na madhara kwa ujumbe huo kwani makao yake makuu huko Naqourra na maeneo ya karibu yameshambuliwa mara kwa mara tangu kuanza kwa mapigano kati ya pande hizo mbili.

Kutokana na mashambulizi hayo, asubuhi ya leo Oktoba 10, walinda amani wawili wa UNIFIL walijeruhiwa baada ya kombora lililorushwa moja kwa moja na Kifaru cha IDF  kuelekea mnara wa uangalizi wa makao hayo makuu ya UNIFIL kusababisha waporomoke na hadi sasa wako hospitali.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wapo kusini mwa Lebanon kuunga mkono kurejea kwa utulivu chini ya mamlaka ya Baraza la Usalama la 2006.

Shambulio lolote la makusudi dhidi ya walinda amani ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na azimio 1701 la Baraza la Usalama, kulingana na UNIFIL, Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon.

Mashambulizi ni mengi

Ongezeko la hivi karibuni la mashambulizi katika msitari wa Blu linasababisha uharibifu mkubwa wa miji na vijiji kusini mwa Lebanon, huku makombora yakiendelea kurushwa kuelekea Israel, yakiwemo maeneo ya kiraia, kulingana na ujumbe huo wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Siku jana Jumatano askari wa IDF walifyatua risasi kwa makusudi na kuzima kamera za ufuatiliaji wa eneo hilo, UNIFIL imesema, na kuongeza kuwa IDF pia ilirusha risasi kwa makusudi UNP 1-32A, ambapo mikutano ya mara kwa mara ya pande tatu ilifanyika kabla ya mzozo kuanza, na kuharibu taa na kituo cha mawasiliano.

"Katika siku zilizopita tumeona uvamizi kutoka Israelndani ya Lebanon huko Naqoura na maeneo mengine," imesema UNIFIL.

Wanajeshi wa IDF wanaendelea kupambana na waasi wa Hezbollah huko nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa UNIFIL wanajeshi wa IDF pia walifyatua risasi kwenye nafasi ya 1-31 ya Umoja wa Mataifa huko Ras Naqoura, na kugonga lango la handaki ambapo walinda amani walikuwa wakilinda na kuharibu magari na mfumo wa mawasiliano.

Imeendelea kusema kuwa ndege isiyo na rubani ya IDF ilionekana ikiruka ndani ya eneo la Umoja wa Mataifa hadi kwenye lango la handaki.

"Tunawakumbusha IDF na wahusika wote wajibu wao wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na mali zao na kuheshimu kutokiukwa kwa majengo ya Umoja wa Mataifa wakati wote," umesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa "Tunafuatilia kwa IDF kuhusu masuala haya."