Vijana 500 kufundishwa uvuvi, kilimo katika Tamasha la Kizimkazi

3 months ago 101

By  Zuleikha Fatawi

Reporter

Mwananchi Communications Limited

Unguja. Vijana 500 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo kupitia tamasha la Kizimkazi, litakalofanyika Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.

Tamasha hilo la Kizimkazi linatarajiwa kuanza Agosti 18, 2024 na litaambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo ufunguzi wa miradi, maonyesho ya vyakula vya asili na michezo.

Akitoa taarifa hiyo leo Julai 28, 2024, Mwenyekiti wa tamasha hilo, Mahfudh Said Omar amesema litakuwa ni fursa kwa vijana kuibua na kuvitangaza vipaji vyao hivyo walitumie vizuri.

"Tamasha hili litakalodumu kwa wiki  moja, litatoa mafunzo kwa vijana 500 na litafungua miradi ikiwemo Akademia ya michezo ya Samia Suluhu Hassan, Ufunguzi wa skuli ya maandalizi, ufunguzi wa dakhalia pia litajumuisha michezo mbalimbali," amesema Mahfudh.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ephraim Mafuru amesema kwa kushirikiana na kamisheni ya Utalii Zanzibar watakuwa na usiku wa utamaduni utakaotoa fursa ya kutangaza utalii wa kiutamaduni.

Amesema usiku huo kutakuwa na vikundi vitakavyoonyesha ujasiriamali wa utamaduni ili kuwavutia watalii.

Pia amesema watatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa lengo la kukuza mnyororo wa thamani wa utalii.

Akitoa historia fupi ya kuanzishwa kwa tamasha hilo, Said Hamad Ramadhani amesema lilianza mwaka 2015 na ilikuwa ni sherehe ya kumuaga Samia Suluhu Hassan baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa hayati John Magufuli.

Mzee Said amesema baada ya kuteuliwa ndipo Mama Samia alipokutana na wananchi wa Kizimkazi na kufanya sherehe ya kumuaga 2016 iliyojulikana Samia Day na ilipofika mwaka 2017 jina likabadilishwa na kuwa Kizimkazi Day.

Amesema Samia aliwaambia wananchi hao siku hiyo itakuwa maalumu ya kukutana kwa wakazi hao ili kujadili maendeleo yao.

Mzee Said amesema kufikia mwaka 2020 ndipo likaanzishwa rasmi Tamasha hilo la Kizimkazi hivyo ametumia fursa hiyo kuwaita wananchi kuja kuona ukarimu na namna wanavyowakarimu wageni.

"Wananchi wa Kizimkazi tunajivunia kumzaa Makamu wa Rais na Rais wa Tanzania wa kwanza mwanamke, ndio sababu ya kuwaita watu kuja wenyewe kuiona hiyo Kizimkazi," amesema Mzee Said

Kilele cha tamasha hilo kitafanyika katika Akademia ya michezo ya Samia Suluhu Hassan na sio Paje kama ilivyozoeleka hapo awali.

Source : Mwananchi

SHARE THIS POST