Nasteyo Sahane Layle, Meneja wa kushughulikia visa vya ukatili wa kijinsia dhidi ya akina mama, watoto na wanawake huko Gode, jimboni Somali mashariki mwa Ethiopia.
11 Oktoba 2024 Afya
Nchini Ethiopia hususan katika jimbo la Somali, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limechukua hatua kusaidia manusura wa ukatili wa kijinsia kuweza kujenga upya maisha yao wakati huu ambapo takwimu za shirika hilo zinaonesha kuwa zaidi ya wanawake na wasichana milioni 370 duniani kote wamekumbwa na ukatili wa kingono wakati wa utoto wao, yaani kabla ya kutimiza umri wa miaka 15.
Sauti hiyo ya Nasteyo Sahane Layle, Meneja wa kushughulikia visa vya ukatili wa kijinsia dhidi ya akina mama, watoto na wanawake hapa Gode, jimboni Somali mashariki mwa Ethiopia akisema kuwa kazi kubwa tunayoifanya ni visa vinavyohusu ukatili wa kingono.
Ni katika video ya UNICEF iliyochapishwa kuonesha kiza kinachokumba watoto wa kike hususan leo ambayo ni siku ya kimataifa ya mtoto wa kike.
Wahudumu katika kituo kushughulikia visa vya ukatili wa kijinsia dhidi ya akina mama, watoto na wanawake huko Gode, jimboni Somali mashariki mwa Ethiopia.
Hapa Gode, UNICEF imeanzisha kituo hicho cha kutoa huduma zote na sasa kimekuwa ni kama eneo salama kwa manusura wa ukatili wa kingono.
Anaonekana mmoja wa wasaka huduma kituoni hapa akifika tayari kupatiwa huduma, sura yake imefichwa ili kuficha utambulisho wako.
Anapatiwa huduma ikiwemo kupimwa mapigo ya moyo na vipimo vingine na kisha kupatiwa dawa.
Nasteyo anasema, “kinachotusikitisha zaidi ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao walibakwa, na sasa mustakabali wao umeharibiwa.”
Pamoja na Nasteyo, wahudumu wengine katika kituo hiki ni Nimo, Faduo, Ifrah na Hamdi, wote wanawake.
Ni kutokana na huduma zao, manusura wanajiona wako salama kwani wanapatiwa huduma za kisaikolojia na nyingine muhimu wanazohitaji.
Na kisha kupata tena uwezo wa kujiamini na kujenga upya maisha yao.