Tuzo la Wakimbizi la Nansen kutoka UNHCR, Mmoja wa washindi wa 2024 wa kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Nada Fadol, anaunga mkono wakimbizi wanaokimbia vita nchini Sudan.
9 Oktoba 2024 Wahamiaji na Wakimbizi
Mtawa kutoka Brazil amekuwa mshindi wa jumla wa tuzo ya mwaka huu ya Nansen ya kusaidia wakimbizi huku wanawake wengine wanne wakiibuka washindi wa kikanda.
Tuzo hiyo inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) inamuenzi mgunduzi wa mnorway Fridtjof Nansen ambaye katika uhai wake alipatia kipaumbele usaidizi kwa wakimbizi.
Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi inasema Mtawa Rosita Milesi, kutoka Brazil amejitolea kwa takribani miaka 40 kutetea haki za wakimbizi. Amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia maelfu ya wakimbizi kupata huduma muhimu kama makazi, chakula, na ajira nchini Brazil.
Mtawa Rosita akiwa mwanasheria, pia amesaidia kubuni sheria za wakimbizi za Brazil zinazohusiana na haki zao kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.
Maimouna Ba, kutoka Burkina Faso akiwakilisha bara la Afrika, mmoja wa washindi wa Tuzo la Nansen UNHCR 2024.
Washindi wa kikanda
Akiwakilisha bara la Afrika, Maimouna Ba kutoka Burkina Faso, amewezesha watoto 100 waliokimbia makazi yao kurejea shuleni na zaidi ya wanawake 400 kujikwamua kiuchumi.
Kutoka bara la Ulaya ni Jin Davod mkimbizi kutoka Syria ambaye amejenga jukwaa la mtandaoni kusaidia waathirika wa kiwewe kuunganishwa na wataalamu wa afya ya akili.
Kwa upande wake mkimbizi kutoka Sudan Nada Fadol anayeishi nchini Misri amepeperusha bendera ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika kwa kusaidia mamia ya familia zilizokimbilia Misri kusaka usalama.
Deepti Gurung anawakilishi ukanda wa Asia-Pasifiki, na ametambuliwa kwa mchango nchini mwake Nepal kwa kusaidia kubadilisha sheria za uraia baada ya kutambua binti zake wawili hawana haki ya uraia, hivyo kufungua njia kwa maelfu ya watu kupata uraia.
Tuzo la Wakimbizi la Nansen ya UNHCR, Mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya 2024, Dada Rosita Milesi wa Brazili.
Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi amesema kuwa wanawake hawa wameonesha nafasi muhimu ambayo wanawake wanaweza kuchukua katika kusaka majawabu ya kibinadamu.
"Wanawake hawa wameonesha uongozi wa kipekee katika jamii zao na hata kubadilisha sera za kitaifa ili kusaidia wakimbizi," amesema Grandi.
Wananchi wa Moldova nao kutunukiwa
Wakati huo huo, watu wa Moldova wanapewa heshima maalumu kwa kuwakaribisha wakimbizi zaidi ya milioni moja kutoka Ukraine licha ya changamoto za kiuchumi walizokabiliana nazo.
Tuzo hizo zitakabidhiwa katika sherehe zitakazofanyika mjini Geneva, Uswisi tarehe 14 Oktoba, zikiongozwa na mwigizaji wa Afrika Kusini Nomzamo Mbatha, na zitaoneshwa mubashara.
Natalia, mwanasaikolojia na mwalimu, akiwasimamia watoto wa Moldova na Ukrainia wakati wa shughuli ya burudani kwenye kitovu cha kucheza na kujifunzia kilichoanzishwa na UNICEF huko Balti, Moldova.
Sherehe hizo pia zitajumuisha maonesho kutoka kwa Kat Graham, mwimbaji wa Moldova Valentina Nafornita, na msanii Emeli Sandé.