Katibu Mkuu Antonio Guterres akutana na manusura wa shambulizi la atomic la Hiroshima na Nagasaki. (Maktaba)

11 Oktoba 2024 Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Oktoba 11 ameipongeza Nihon Hidankyo, shirika la Kijapani la kupinga silaha za nyuklia kwa kuptunukiwa Tuzo la Amani la Nobel.

Harakati hiyo ya mashinani ya watu walionusurika katika shambulio la bomu la atomiki la mwaka 1945 huko Hiroshima na Nagasaki, inajulikana kama hibakusha, na imejitolea kufikia ulimwengu usio na nyuklia.

Bwana Guterres amewataja hibakusha kama "mashuhuda wasio na ubinafsi, wenye utu na ambao wanashuhudia gharama mbaya za kibinadamu zinazosababishwa  silaha za nyuklia."

Ingawa idadi yao inaendelea kupungua kila mwaka, kazi yao isiyo na kikomo na uvumilivu wao ni "uti" wa harakati za kimataifa za kukomeswha kwa silaha za nyuklia, ameongeza Guteress.

Katibu Mkuu amesema hatasahau kamwe mikutano yake mingi na hibakusha kwa miaka mingi.

Hamasa ya kimataifa

“Ushuhuda wao wa kuogofya unaonesha ulimwengu kwamba tishio la nyuklia halijabaki tu kwenye vitabu vya historia. Silaha za nyuklia bado ni hatari wazi na ya sasa kwa binadamu, inayodhihirika katika lugha ya kila siku ya uhusiano wa kimataifa,” amesema Guterres.

Aidha Gutress amesema,“ni wakati wa viongozi wa dunia kuwa na mtazamo wa wazi kama hibakusha, na kuona silaha za nyuklia kama zilivyo: vifaa vya kifo ambavyo havileti usalama, kinga, au ulinzi. Njia pekee ya kuondoa tishio la silaha za nyuklia ni kuziondoa kabisa.”

Kwa kuhitimisha, Guteress amesema  kwamba Umoja wa Mataifa unajivunia kusimama pamoja na hibakusha ambao “ni chanzo cha hamasa katika juhudi zetu za pamoja za kujenga ulimwengu ulio huru kutoka kwa silaha za nyuklia.”