MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)iliyo chini ya Wizara ya Afya, imetoa taarifa kwa Umma ufafanuzi kuhusu uvumi juu ya Dawa ya Paracetamol inayodaiwa kubabua ngozi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa Umma liyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo Imebainisha kuwa, imebaini uwepo wa taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa dawa aina ya Paracetamol ambayo imeandikwa P 500 na
kudaiwa kubabua ngozi kama inavyooneshwa (pichani).
Akinukuu taarifa hiyo inayosambazwa mitandaoni:
"Dawa hiyo inadaiwa kuwa ni ‘’paracetamol mpya nyeupe sana na inayong'aa, madaktari
wanashauri kuwa ina virusi vya "Machupo", inayochukuliwa kuwa moja ya virusi
hatari zaidi ulimwenguni, na kiwango cha juu cha vifo.
Aidha, Mtoa taarifa anaitaka jamii kuisambaza taarifa hii kwa kila mtu aliyeko katika orodha
yake ya mawasiliano ili kuokoa maisha. Anamalizia kwa kusema ‘’Nimefanya
sehemu yangu, sasa ni zamu yako. Kumbuka kwamba Mungu huwasaidia wale
wanaosaidia wengine. ‘’Sambaza kama ilivyopokelewa’’.
Dkt.Fimbo ameeleza kuwa, Taarifa hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara na TMDA imekuwa ikitolea ufafanuzi ikiwemo taarifa ya mnamo tarehe 10 Mei, 2023, juu ya dawa aina ya P-500®
(PARACETAMOL) ya Apex Laboratories Private Limited, Tamil Nadu, India
iliyodaiwa kuwa na virusi hivyo.
"TMDA inapenda kuufahamisha Umma kwa mara nyingine kwamba hakuna virusi
vinavyojulikana kwa jina la Machupo. Aidha, virusi vya aina yoyote haviwezi kuishi kwenye kidonge.
Dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu
zilizopo katika soko nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara zimesajiliwa baada
ya kuthibitishwa kuwa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi unaotakiwa na
hivyo, ni salama kwa matumizi yaliyoainishwa.
Katika hatua hiyo, TMDA inapenda kuwahakishia wananchi kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake wa
kulinda afya ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa bidhaa tiba zinazotumika nchini ni zile
zenye kukidhi matakwa ya ubora, usalama na ufanisi.
Vilevile, Mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kupata ufafanuzi
kutoka kwenye mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zinazoweza kuleta
taharuki kwenye Jamii.
TMDA yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa tiba nchini ambapo Ili kuhakikisha kuwa bidhaa tiba (zikiwemo dawa) zilizoko katika soko nchini zinakidhi matakwa ya usalama, ubora na ufanisi, TMDA imeweka mifumo mbalimbali ya udhibiti ikiwa ni pamoja na tathmini na usajili, ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara na ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa katika soko.
Aidha, Wananchi wanaweza kupiga simu ya bila malipo: 0800110084 endapo wapatapo taarifa za mashaka kama hizo.