Straika Coastal apiga hesabu za Simba

3 months ago 41

By  OMARY MDOSE

Reporter

Mwnananchi Communications Limited

WAKATI safu ya ulinzi ya Simba ikiongozwa na beki Mcameroon, Che Malone Fondoh ikiwa haijaruhusu bao lolote katika mechi nne za Ligi Kuu Bara msimu huu, imeonekana kumpa kazi mpya mshambuliaji wa Coastal Union, Maabad Maulid, akianza kupuiga hesabu kali kabla ya kesho timu hizo kukutana.

Maabad  ndiye mshambuliaji kinara wa Coastal, akiwa na mabao mawili na tuzo moja ya Mchezaji Bora wa Mechi aliyoipata dhidi ya Pamba Jiji, amesema anafahamu ana kazi ngumu inayomkabili mbele ya safu ya ulinzi ya Simba, lakini ana dawa yao.

Kauli ya Maabad imekuja kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara unaokwenda kuzikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maabad amesema baada ya kutoka kucheza dhidi ya Pamba Jiji, kazi kubwa aliyonayo ni kuboresha zaidi kiwango chake na mbinu za kuwapita mabeki ili azidi kufanya vizuri zaidi.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa KVZ FC ya Zanzibar, amesema ili kukabiliana na mabeki wagumu kama wale wa Simba akiwemo Che Malone lazima uwe vizuri kiakili na kisaikolojia.
“Mchezo ujao tunakwenda kucheza na Simba ambayo ni timu kubwa, huwezi kuzitaja timu kubwa Afrika ukaiacha, hivyo lazima tujipange kisawasawa tunapokwenda kukabiliana nayo.

“Mimi ni mshambuliaji na jukumu langu ni kufunga, lakini nafahamu naenda kukutana na mabeki ambao wametoka kuisaidia timu yao kufanya vizuri mashindano ya kimataifa.

“Kutokana na hilo, lazima nijipange kukabiliana nao kiakili na kisaikolojia ili nifanikishe malengo yangu, haitakuwa rahisi lakini dawa ya kufanya vizuri dhidi yao ninayo,” alisema mshambuliaji huyo.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST