Sikuwahi kuota kushiriki Olimpiki – Perina, mkimbizi kutoka Sudan Kusini

3 months ago 54

Perina ambaye familia yake ilikimbia vita Sudan Kusini akiwa na umri wa miaka 7 na kufika kambi ya Kakuma nchini Kenya alieleza hayo wakati akiwa kwenye mazoezi ya mbio huko Eldoret, Kenya, eneo la muinuko wa zaidi ya 2100 ambalo hupendwa sana kutumiwa na wanamichezo kutokana na kuwajengea uthabiti wa pumzi wakiwa kwenye mashindano.

Sasa ana umri wa miaka 21 na timu yao ya wakimbizi inafadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR. Yeye ni mwanaridha pekee kutoka Afrika katika timu hiyo ya wakimbizi.

“Nitakapomaliza mbio na kushinda, nitampigia simu mama yangu na kumwambia nimeweza! Nitakuwa nimefanikiwa na hivyo ninaweza kurejea nyumbani na kusaidia familia yangu,” anasema Perina.

Muhimu ni mazoezi hata kama ni magumu kiasi gani

Katika video hii ya UNHCR Perina yuko makini kila siku ya mazoezi, hapa anaonekana akijiandaa kukimbia na kuweka muda kwa kutumia saa yake.  Katika mazoezi haya hapa Eldoret yuko na wenzake wanaomuunga mkono.

Jambo muhimu kwa Perina ni mazoezi, “mazoezi tu,  nataka kujikita kwenye mazoezi. Hata yawe magumu kiasi gani, lazima niendelee. Nitaendelea na mazoezi bila malalamiko ili niweze kuwa katika hali nzuri.”

Awali Perina alijaribu mpira wa miguu au kabumbu, vile vile mpira wa kikapu, lakini rafiki yake mmoja alimshauri aingie kwenye kukimbia.

Mwalimu wa Perina ni bingwa wa Olimpiki Janet kutoka Kenya

“Tumekuwa tunajiandaa kiakili na kimwili, hasa kwa kujenga uthabiti kupitia mazoezi,” anasema Janeth Jepkosgei, bingwa wa zamani wa michezo ya Olimpiki kutoka Kenya ambaye kwa sasa ndiye kocha wa Perina.

Janeth anasema Perina amekuwa anafanya mazoezi kwa bidii tangu kukimbia mita 800 kwa dakika 2 na sekunde 29 hadi kufikia muda bora zaidi kwake wa dakika 2 na sekunde 12 wakati wa majaribio ya kitaifa.

Matumaini ya Janeth ni kwamba Perina atang’aa jijini Paris na kwamba ataboresha zaidi muda wake huo wa kukimbia kwa kiasi kikubwa, pengine hata kuvunja rekodi yake mwenye ya dakika 2 na sekunde 12.

Kila siku saa 11 alfajiri yeye na wenzake hufanya mazoezi ya kukimbia kilometa 20. Ushindi wake kwenye mashindano ya riadha mwaka 2022 yalimwezesha kupata usaidizi wa masomo kwenye shule ya Shoe4Africa iliyoko kaunti ya Nandi, kilometa 350 kutoka mji mkuu wa Kenya, Nairobi, shule iliyoanzishwa na mwanariadha maarufu duniani wa mbio za nyika kutoka Kenya, Mary Keitany.

Ndoto ya kushiriki Olimpiki haikuwahi kuwa sehemu ya ndoto zake

“Katu sikuwahi kufikiria kuingia michezo ya Olimpiki,” anasema Perina akiongeza kuwa, “tulipokuwa kwenye majaribio ya Olimpiki, muda wangu bora ulikuwa dakika 2 na sekunde 12. Hivyo natumaini kumaliza mbio dakika 2 na sekunde 10.”

Perina ambaye hadi sasa anasoma elimu ya juu ya sekondari, anasema timu yake anayoshiriki nayo kwenye mazoezi wako kama ndugu tu kwani “tunafanya mazoezi pamoja na wanafurahia kuwa nitashiriki kwenye Olimpiki. Nitakapoenda kwenye michezo ya Olimpiki, nitajaribu kulenga muda wangu bora zaidi ili timu yangu iweze kutambuliwa zaidi.”

Nikishinda nitalipia ndugu zangu karo za shule

Kando ya kutaka kuinua timu yake, Perina anawazia pia ndugu zake na mama  yake akisema, “mimi ni mzaliwa wa kwanza kwenye familia yetu, wengine bado ni wadogo. Iwapo nitafanya vema, nataka kusaidia kulipia karo za shule wadogo zangu. Ningependa pia kumhamisha mama yangu kutoka kambi ya Kakuma na kumleta hapa Eldoret. Nitamnunulia nyumba ambamo ataishi.”

Na Perina hafichi furaha na shukrani kwa mola wake akisema “nina furaha sana. Namshukuru Mungu amenitoa mbali. Nina furaha sana.”

Source : UN Habari

SHARE THIS POST