Muktasari:
- Majaliwa ameagiza Wizara ya Afya kuendelea kushirikiana na wadau wa michezo kwa lengo la kufikisha elimu ya kufanya mazoezi kwa Watanzania.
Dodoma. Jumla ya Sh300 milioni zimepatikana katika marathoni iliyoandaliwa na Benki ya NBC, zitakazosaidia masuala ya afya, ikiwamo saratani ya shingo ya kizazi.
Pia, fedha hizo zitafadhili mafunzo kwa wakunga, ili kuboresha afya ya mama na mtoto na kusaidia kufadhili chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili.
Akizungumza leo Jumapili Julai 28, 2024 katika mbio za NBC marathon, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema benki hiyo imetenga katika bajeti yake Sh32.6 bilioni kwa ajili ya kuthamini michezo mbalimbali, ikiwamo ligi kuu ya mpira wa miguu na marathoni hiyo.
“Tendo lenu la kuendelea kuwekeza usimamizi katika michezo, huu ni mkakati tunauona wa uwazi kabisa wa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanamichezo namba moja nchini anayehamasisha na kuheshimisha michezo,”amesema Majaliwa.
Amesema kutokana na marathoni hizo, jumla ya Sh300 milioni zimekusanywa na kukabidhiwa kwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa ajili ya mapambano ya saratani ya shingo ya kizazi na nyingine Hospitali ya Benjamin Mkapa na Muhimbili.
Pia, Majaliwa ameagiza Wizara ya Afya kuendelea kushirikiana na wadau wa michezo kwa lengo la kufikisha elimu ya kufanya mazoezi kwa Watanzania.
“Watanzania wanaendelea kuhamasishwa kubadilisha mitindo ya kuishi, kuepuka tabia zembe zinazochochea magonjwa yasiyoambukiza, tuendelee kuzingatia mazoezi ya kila aina,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema kila mtu anatakiwa kutembea hatua 10,000 kwa siku.
“Sasa pale mahali unapoweza kutembea, tafadhali epuka bodaboda, bajaji na usafiri mwingine, tembea ili kufikisha hatua hizo,” amesema Profesa Janabi.
Amesema miongoni mwa faida ambazo mtu atapata akifanya mazoezi ni kukingwa na maradhi ya moyo, kuongeza afya ya akili, kukingwa na kisukari na wale wenye ugonjwa huo itasaidia kuudhibiti.
Hata hivyo, amesema kufanya mazoezi tu bila kuangalia chakula unachokula kila siku hakutaleta matokeo mazuri ya kiafya.
Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Hamis Mwijuma amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wameunda kamati kwa lengo la kuhakikisha shughuli za michezo zinafanyika nchi nzima.
“Kamati inaendelea kufanya shughuli hiyo ya kuandaa utaratibu wa namna ambayo shughuli hii inaweza kufanyika na hivi karibuni tutatoa matokeo yake na kutoa maelekezo ya namna ambavyo kuanza shughuli za michezo katika wilaya zote nchini,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amesema mbio hizo kwa mara ya kwanza zilifanyika Novemba 11, 2020 na walifanikiwa kupata wakimbiaji 1,944 na kukusanya Sh100 milioni.
Hata hivyo, amesema mbio hizo zimeendelea kukua mwaka hadi mwaka, kwa kuhusishwa wakimbiaji kutoka nchi mbalimbali na kwa mwaka huu zaidi ya watu 8,000 wameshiriki.
Amesema kwa muda wa miaka minne ya mbio zimekusanywa Sh700 milioni ambazo zimeelekezwa katika mapambano ya shingo ya kizazi na ufadhili wa mafunzo kwa wakunga.
Amesema fedha hizo ziliwezesha uchunguzi kwa wanawake 45,000 huku wanawake 1,500 waliokutwa na saratani hiyo wakitibiwa bure na 80 kati ya waliotibiwa wamepona.
Pia, amesema wakunga 100 wamepata mafunzo kwa lengo kupunguza vifo vya mama na mtoto na programu hiyo wanaifanya kwa kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Amesema kati ya Sh300 milioni zilizokusanywa leo, Sh100 milioni zitaelekezwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Sh100 milioni zinaelekezwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya mafunzo ya wakunga 100.
Amesema Sh50 milioni zinaelekezwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuchangia ujenzi wa wodi ya upasuaji.