Rais Samia ataka ushirikiano Serikali, sekta binafsi kuboresha huduma za afya

1 month ago 9

By  Jesse Mikofu

Mwandishi wa Habari

Mwananchi

Muktasari:

  • Uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi, upungufu wa vifaatiba na uchakavu kwa baadhi ya miundombinu ni changamoto zinazoikabili sekta ya afya

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amesema licha ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali kuboresha huduma za afya kwa wananchi bado kuna changamoto ya utoaji huduma, hivyo ushirikiano wa sekta binafsi utasaidia kuziimarisha.

Ametaja changamoto hizo kuwa ni uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi, upungufu wa vifaatiba na uchakavu kwa baadhi ya miundombinu.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba mosi, 2024 kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 11 la Afya Tanzania (THS) lililofanyika Fumba, wilayani Magharibi B, Unguja.

Kongamano hilo limewakutanisha wataalamu zaidi ya 1,500.

“Ni vyema mkafahamu pamoja na hatua zinazofikiwa bado kuna changamoto katika utoaji wa huduma, hivyo Serikali itaendelea kushirikisha sekta binafsi katika kutoa huduma kwa wananchi ambao ushirikiano huo unakusudia kuimarisha huduma bora za afya nchini,” amesema Rais Samia.

Amesema Serikali itaendelea kuboresha elimu kwa wataalamu wa afya kwa kutoa kipaumbele na kuongeza ufadhili kwa mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi katika taaluma za kimkakati.

Kuna umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Rais Samia amesema Serikali zote mbili zinaendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya utoaji wa taarifa ili iweze kusomana kutoka kituo kimoja cha afya kwenda kingine katika ngazi zote za utoaji wa huduma kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa za wagonjwa, zikiwamo vipimo na matibabu.

Pia, kutoa fursa ya kupata matibabu zaidi katika maeneo yote ya nchi.

“Serikali zote (SMT na SMZ) zinaendelea kuchukua hatua za kuimarisha huduma za kinga, kuwekeza katika miundombinu ya afya kwa kujenga na kukarabati hospitali zote na vituo vya afya ili ziweze kutoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano,” amesema Rais Samia.

Ametoa wito kwa taasisi za Serikali na binafsi kushirikiana na THS kuongeza nguvu ya majadiliano katika sekta ya afya na kuboresha utoaji huduma za afya mijini na vijijini.

Awali, akitoa taarifa ya kitaalamu kwa niaba ya bodi ya THS, Dk Grace Magembe amesema imekuwa ni chachu ya kuleta mabadiliko endelevu katika sekta ya afya hasa katika kuhamasisha utoaji huduma kwa mifumo ya kidijitali ili kuendana na wakati.

Dk Grace amesema THS imewawezesha vijana kupitia programu ya kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo, kuwaendeleza kitaaluma na kuwaunganisha watumishi wa afya na fursa zilizopo nje ya nchi.

“THS ina jukumu kubwa la kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuboresha na kuimarisha sekta hasa katika eneo la kutoa elimu ya afya kwa jamii,” amesema Dk Grace.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amezikaribisha sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kujenga huduma za kibingwa ili kuifanya Tanzania kuwa kituo cha utalii wa tiba.

Amesema bado Serikali inahitaji ushirikiano na sekta binafsi katika maeneo mbalimbali.

Kuhusu bima ya afya kwa wote, Jenista  amesema Serikali inapokwenda katika utekelezaji, sekta binafsi inapaswa kushirikiana nayo kwa kuhakikisha huduma bora na rahisi zinapatikana.

“Pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali lazima kuhakikisha sekta binafsi inaimarishwa ili kulinda usalama wa wananchi,” amesema.

Waziri wa Afya Zanzibar, Ahmed Mazrui amesema ubia wa sekta binafsi umekuwa na mafanikio makubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya vifaatiba vya kisasa.

Amesema hospitali binafsi zimewekeza na kuhakikisha zinatoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri Mazrui amesema changamoto zilizopo zinaendelea kushughulikiwa hatua kwa hatua hivyo zinazidi kupungua.

Amesema wameimarisha vituo vya afya ya msingi 52 na kujenga vipya 96 ili kufikia mwakani huduma za afya ziwe bora zaidi kwa wananchi.

Source : Mwananchi

SHARE THIS POST