Shirika la Posta Tanzania na huduma za kidijitali
9 Oktoba 2024 Malengo ya Maendeleo Endelevu
Leo siku ya posta duniani huduma ambayo ilionekana kuwa itasambaratika kufuatia ujio wa maendeleo ya teknolojia ya intaneti lakini wenyewe wasimamizi wa huduma hii duniani wanasema licha ya mtikisiko sasa mambo yanashamiri, siri kubwa ikiwa ni ubia badala ya ushindani.
Tunasherehekea miaka 150 ya shirika la Umoja wa Mataifa la Posta, UPU, tunatambua umuhimu wa moja ya mifano ya mapema zaidi ya ushirikiano wa kimataifa. Ni Masahiko Metoki, Mkurugenzi Mkuu wa UPU katika ujumbe wake wa siku hii adhimu akiongeza kuwa, « kile kilichoanza na wanachama 22 sasa inajumuisha nchi 192, kikionesha uthabiti wa ushirikiano wa kimataifa.”
Akaendelea kusema kwamba wamekumbana na changamoto, vita, majanga mabadiliko ya kasi ya teknolojia ya kidijitali.
“Leo hii UPU inaongoza juhudi za kufanya huduma za posta kuwa za kisasa na bora. Inatoa fursa kwa nchi kushirikishana ufahamu, kusaka majawabu na kukabili changamoto za sasa. Moyo wetu wa ushirikiano ndio umetusaidia kugeuza vikwazo kuwa fursa na kufanya huduma za posta kuendana na dunia inayobadilika.”
“Pale ambapo awali tuliona ongezeko la mawasiliano ya kidijitali na kupungua kwa kiwango cha utumaji wa barua kwa njia ya posta kama tishio, sasa tunaona fursa za utajiri. Mtandao mkubwa wa UPU umesaidia kupanuka kwa huduma mbali mbali ikiwemo biashara mtandao, huduma za kifedha, kijamii na kidijitali, ikihakikisha ufikiaji wa kila mtu duniani hata wale walio ndani zaidi hawaachwi nyuma.”
Mkurugenzi Mkuu huyo wa UPU amesema badala kuona ushindani kama changamoto, UPU inakaribisha wadau mbali mbali. Mtazamo jumuishi unaimarisha uwezo wao kukabili changamoto kama vile mabadiliko ya tabianchi, ambayo yanahitaji ushirikiano mipakani.
Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, UPU imehimili changamoto kwa kuwa bunifu, jumuishi na kusongesha ushirikiano wa kimataifa.
“Katika siku hii muhimu, hebu na tusherehekee na tupongeze kazi ya shirika la Posta duniani ya kuondoa umbali na kuunganisha dunia.”