Mwananchi Communications Limited
Muktasari:
- Pamba Jiji itacheza mchezo huo wa saba kwao katika ligi msimu huu wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 12:30 jioni.
KOCHA Msaidizi wa Pamba Jiji, Henry Mkanwa, ameyataja mambo mawili ambayo wataingia nayo kesho Alhamisi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga.
Pamba Jiji itacheza mchezo huo wa saba kwao katika ligi msimu huu wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 12:30 jioni.
Katika mechi sita zilizopita, Pamba Jiji imekusanya pointi nne zilizotokana na sare nne, huku ikipoteza mbili, haijashinda hata moja.
Kwa upande wa Yanga, huo ni mchezo wa nne baada ya kushinda yote iliyotangulia ikifunga jumla ya mabao manne huku ikiwa haijaruhusu bao.
"Kimbinu kesho tunakwenda kucheza mpira wa kushambulia na kuzuia, sio kujilinda muda wote.
"Lolote linawezekana, unapocheza mechi yoyote unategemea matokeo ya aina tatu, kushinda, droo au kufungwa, lakini kesho nataka matokeo mawili ambayo ni kushinda au droo," alisema kocha huyo na kuongeza.
"Mpango wetu uko vizuri, kesho tunakwenda kupambana kupata matokeo mazuri, Mungu akijaalia tunaweza kuondoka na ushindi. Mimi na vijana wangu hatuna presha yoyote. Tutaingia uwanjani kwa kuwaheshimu Yanga kwani ni timu bora na sisi tunajiandaa kucheza mpira mzuri na kupata matokeo mazuri."
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wa Pamba Jiji, kiungo wa timu hiyo, Paulin Kasindi raia wa DR Congo, amesema: "Tunajiandaa vizuri kabisa kwa sababu tunajua Yanga ni timu ya aina gani, hivyo tunaiheshimu na tuko tayari kupambana nao.
"Hatuna hofu kwa sababu ukiangalia baadhi ya wachezaji wa Pamba wameshawahi kucheza dhidi ya Yanga pamoja na timu zingine kubwa za hapa Tanzania, mechi ni mechi, dakika tisini zitakapoisha tutajua nani mshindi. Mimi binafsi nishacheza nao nikiwa Coastal na Tabora, tutapambana nao, hakuna hofu yoyote.
"Msione kama tunakuja kwa ajili ya kuipatia Yanga pointi tatu, hapana, kila mmoja lazima akipambanie chake kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana."
Kuhusu mipango yao ya kusaka ushindi wa kwanza, kiungo huyo alisema: "Mshindi siku zote akianguka mara tisa, lazima apambane ile ya kumi ainuke, hivyo kutopata ushindi katika mechi sita za kwanza haitufanyi tukate tamaa, tutapambana kufikia malengo yetu."