Muktasari:
- Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamehama na waliobaki wanaishi kwa hofu kwa kuwa maji bado yanaongezeka.
Kigoma. Si ajabu Ziwa Tanganyika kuongezeka kina cha maji kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mvua, lakini hali ni tofauti kwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa takwimu za mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika, mvua zilizonyesha Mkoa wa Kigoma, kiwango cha maji ziwani kiliongezeka kutoka usawa wa bahari hadi mita 777.17 Aprili mwaka huu ikilinganiswa na mita 776.35 Mei 2023 na mita 776.27 Mei 2022.
Kuongezeka kwa kina cha maji kulichangiwa kwa kuongezeka kwa kiwango cha mvua kwa wastani wa asilimia 28 hadi kufikia milimita 1,071.9 mwaka 2023/24 ikilinganishwa na milimita 836.8 miaka miwili iliyopita.
Kutokana na ongezeko hilo la mvua, maji yalijaa maeneo mengi mkoani Kigoma.
Hata hivyo, awali mamlaka husika zilieleza maji yangeweza kufika katika maeneo yaliyo karibu na ziwa hilo, hivyo kuleta athari kwa wananchi.
Miongoni mwa maeneo hayo, ni Mtaa wa Mgumile uliopo Kata ya Kagera, Manispaa ya Kigoma Ujiji, uliokumbwa na mafuriko na kusababisha makazi na mashamba ya watu kusombwa.
Kata hiyo inayokadiriwa kuwa na wakazi 9,916 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, robo ya wakazi wake, maeneo yao yalizingirwa na maji.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamehama na waliobaki wanaishi kwa hofu kwa kuwa maji bado yanaongezeka.
Malilo Zaidi, aliyekaa Mtaa wa Mgumile tangu mwaka 1983 anasema, “hali hii haijawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 40, Serikali inapaswa kuangalia suala hili kwa undani na kutupatia maeneo mengine ya makazi na kilimo.”
Mwaka huu yameshuhudiwa mafuriko yaliyoharibu makanisa, hospitali, shule, barabara, masoko, hoteli na maeneo ya fukwe huku baadhi ya wananchi kukosa makazi.
Jalala Shabani, mama wa watoto tisa anayeishi kwenye nyumba ya nne sasa kwa kuhama mara kadhaa, baada ya kukimbia maji yanayoongezeka.
Hali hii imemlazimu kupika kwa jirani na kuwabeba watoto wake kwenda kulala usiku huko.
“Ninaishi na mume wangu na watoto, maji yalianza kwenye nyumba ya kwanza tukasogea kukimbia maji tukahama lakini kila tukisogea na kuhama maji nayo yanasogea,”anasema Jalala.
Anasema maji yameharibu nyumba zao, vifaa vya ndani na mashamba ya mchikichi, mahindi na maharagwe.
Jalala anasema kwa sasa anategemea vibarua kuendesha maisha, hali ambayo imerudisha nyuma maendeleo yake.
“Kukosa huduma za kijamii kama shule, hospitali na makanisa, kumetuathiri sana na baadhi ya watoto wangu hawajakwenda shule kwa miezi minne sasa.
“Ninaiomba Serikali msaada wa makazi na huduma za kijamii ili kukabiliana na hali hii ngumu,” Jalala.
Mjumbe wa Mtaa wa Mgumile, Ukiwa Sadi ameathirika na mafuriko yaliyoharibu biashara yake ya chakula maarufu kama mamantilie.
Sadi aliyekuwa na kibanda akiuza chakula nyumbani kwake, maji yaliingia na kuharibu mali na bidhaa zake zote za biashara.
“Hii ilinilazimu kuhama na kuendeleza maisha sehemu nyingine. Ingawa nimejaribu kujipanga upya na kuanza kupika tena, hali ya kibiashara ni mbaya kutokana na ukosefu wa wateja,” anasema Sadi.
Anasema mtaji wake umepungua kwa kuwa amekuwa akinunua mchele kilo tano hadi kumi na kuuza, ikilinganishwa na kilo 100 za awali.
Afya na usalama
Zainabu Sabuni anasema maisha yao yamekuwa hatarini kwa kutumia maji ya visima ambayo si salama.
Anasema wamekuwa wakihofia magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na homa za matumbo.
Zainabu anasema wamekuwa wakitumia maji hayo kwa kunywa na matumizi mengine, huku wakihofia magonjwa ya ngozi na minyoo.
Anasema visima hivyo, vimechimbwa baada ya kukosa maji kwa muda mrefu.
Baadhi ya wakazi wananunua majisafi kwa Sh1,500 kwa ndoo, lakini wengine wanatumia maji ya visima kwa kukosa uwezo wa kununua.
Zena Haruna, anasema usalama wao unatishiwa na wanyama wakali kama viboko kuvamia makazi, kujeruhi watu na kuua mifugo.
“Tunaishi kwa wasiwasi na kuhofia usalama wetu kutokana na wanyama wanaokuja hasa nyakati za usiku kutafuta chakula na kufanya uharibifu,”anasema Zena.
Diwani wa Kagera, Gregory Kebelezo anasema Mtaa wa Mgumile umekumbwa na mafuriko makubwa, yakiathiri kaya 60 kati ya 306 na kusababisha wakazi kuhama.
Vitu vilivyoathiriwa anasema ni mashamba ya michikichi, mpunga, mahindi na maharagwe.
“Shule pia zimejaa maji, watoto wameshindwa kusoma. Ofisi ya mkurugenzi wa manispaa imepanga eneo lingine kwa ajili ya ujenzi wa shule. Hakuna vifo vilivyotokea, lakini mali na makazi yameharibiwa na wakazi wameathirika kiuchumi,”anasema Kebelezo.
Pia, huduma ya majisafi imeathirika kutokana na kujaa kwa Mto Luiche na uharibifu wa miundombinu, inayosubiri kurekebishwa na wataalamu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (Kuwasa).
Uvuvi na biashara
Suala la usafirishaji na biashara katika Bandari Ndogo ya Kibirizi, mkoani Kigoma limeathiriwa na ujazo wa kina cha maji katika Ziwa Tanganyika.
Licha ya Serikali kuwahamishia wafanyabiashara wa samaki na dagaa kwenye eneo jipya, lakini wamepoteza wateja na biashara zao kuyumba.
Zabibu Hussein, mfanyabiashara wa dagaa anasema pamoja na kuhamia soko jipya mauzo yameshuka.
“Tumepoteza wateja, soko hili watu hawajalizoea. Tunapata mawazo kwa kuwa fedha za mitaji zenyewe tulikopa,”anasema Zabibu.
Selina Jeremia anasema licha ya kwamba hakuna wateja kwenye soko hilo, anaoimba Serikali isiwahamishe tena kwa kuwa kuhamahama imekuwa kero kwa biashara zao.
“Eneo hili lipo kwenye mwinuko, tunaiomba Serikali ituache hapa wateja watazoea,” anasema Selina.
Kata ya Katubuka, Manispaa ya Kigoma Ujiji, pia ni moja ya eneo ambalo maji yamejaa na kusababisha mafuriko katika makazi ya watu na vibanda vya biashara.
Mfanyabiashara Harrison Kinoni anasema mabucha ya nyama ya nguruwe yameathirika na wateja wamepungua. “Tumehamia upande wa pili wa barabara, lakini biashara imekuwa ngumu, awali tuliuza hadi nyama ya nguruwe watatu kwa siku lakini sasa hata nguruwe mmoja haishi,”anasema Kinoni.
Diwani wa Katubuka, Moshi Mayengo anasema nyumba zaidi ya 60 zimezungukwa na maji, hali iliyowahi kutokea mwaka 1989/90.
Mayengo anasema Serikali ya mkoa ipo kimya, licha ya jitihada zake za kuwasiliana na Wakala ya Barabara za Vijijinina Mijini (Tarura), hakuna hatua zilizochukuliwa.
Kauli ya Bonde la Ziwa Tanganyika
Mhandisi Odemba Kornel kutoka Bonde la Ziwa Tanganyika, anasema mwaka 2024, kipimo cha maji ziwani kimefikia mita 777.22 kutoka usawa wa bahari, kikilinganishwa na mita 747 mwaka 2018, kutokana na mvua kubwa.
“Mabadiliko ya tabianchi yanasababisha maji kujaa na kupungua, historia inaonesha hali kama hii ilitokea miaka ya 1960. Tunashauri wananchi kuepuka uwekezaji au shughuli za kimaendeleo karibu na ziwa ili kuepuka hasara,”anasema Kornel.
Anasema wawekezaji na wadau wanashauriwa kuchukua takwimu za maji kutoka ofisi za bonde kabla ya kuanza miradi.
Kornel anasema Bonde la Ziwa Tanganyika limeweka alama kuonesha maeneo hatarishi na wataendelea kufanya hivyo.
Anasema wana mpango wa kuzunguka tena katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika baada ya maji kuongezeka zaidi kuliko awali ili kuweka alama na kuwapa tahadhari wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye anasema Wilaya ya Kakonko nyumba za mitaa 20 ziliharibika kutokana na mvua kubwa.
“Serikali ilitoa misaada ya kibinadamu. Pia katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, eneo la Kata ya Katubuka limezungukwa na maji na wataalamu bado wanachunguza chanzo cha mafuriko hayo,” anasema Andengenye.
Bandari Ndogo ya Kibirizi, Soko la Mwalo wa Kibirizi na Chuo cha Maendeleo ya Uvuvi (Feta) vimeathirika na kuongezeka kwa maji ya Ziwa Tanganyika.
Wilaya ya Uvinza pia imeathirika, Kivuko cha Ilagala kimesimama kutokana na mafuriko ya Mto Malagarasi.
Andengenye anasema Serikali haina nia ya kupoka maeneo ya wananchi, lakini inawashauri kuepuka kujenga makazi katika maeneo hatarishi.
Pia, anawataka wazazi kuwapeleka watoto shule katika maeneo salama wakati Serikali ikiendelea kutafuta suluhisho ili wananchi waendelee na maisha yao kwa usalama.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation