OHCHR yalaani vikali kuendelea kushika kasi machafuko Mashariki ya Kati

1 month ago 15

Katika ombi la kutaka kukomeshwa kwa "mauaji, uharibifu na mipango ya vita na wale walio madarakani”, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imesema kwamba “hali kwa raia wa nchini Lebanon, Gaza, Israel na Syria inazidi kuwa mbaya siku hadi siku”.

Leo Ijumaa Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL kimeripoti kwamba walinda amani wawili wamejeruhiwa "baada ya milipuko miwili karibu na mnara wa uchunguzi. Jana Alhamisi, jozi ya wanajeshi wa kikosi hicho pia walijeruhiwa baada ya Kifaru cha kikosi cha Israel IDF Merkava kufyatua silaha yake kuelekea mnara wa uchunguzi katika makao makuu ya UNIFIL huko Naqoura, na kuupiga moja kwa moja na kuuafanya kuanguka", imesema ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Ofisi hiyo imeongeza kuwa "Matukio haya yanawaweka tena walinda amani wa Umoja wa Mataifa, ambao wanahudumu kusini mwa Lebanon kwa ombi la Baraza la Usalama chini ya azimio 1701 (2006), katika hatari kubwa."

Mashambulizi makubwa Beirut

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi na waandishi wa habari hii leo  msemaji wa OHCHR Ravina Shamdasani ameelezea jinsi mji mkuu wenye wakazi wengi wa Beirut "unavyozidi kukumbwa na mashambulizi ya anga ya Israel ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya 2,100 katika mwaka uliopita, kulingana na mamlaka ya Lebanon.”

Msemaji huyo wa OHCHR amebainisha kwamba hatua hiyo inakuja wakati Hezbollah na makundi mengine yenye silaha "yanaendelea kurusha maroketi Kwenda nchini Israel, na kusababisha vifo vya kwanza vya raia kaskazini mwa nchi hiyo tangu kuongezeka kwa uhasama kati ya Israel na Lebanon mwezi uliopita,"

Ameelndelea kusema kuwa vituo vya huduma za afya na wafanyikazi wa dharura hawajanusurika kutokana na mashambulizi  yanayozidi kuongezeka ya Israeli, huku vituo 96 vya huduma za afya na zahanati zikifungwa kufikia tarehe 5 Oktoba, imesema mamlaka ya Lebanon.

"Tumekuwa na ripoti kadhaa pia za mashambulizi ya anga, yakilenga vituo vingine vya matibabu na wahudumu wa afya pamoja na wazima moto, kuuawa," amesema Bi. Shamdasani.

Tangu tarehe 30 Septemba, wafanyakazi 49 wa huduma  za afya wameuawa katika mashambulizi tisa yaliyothibitishwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO.

Nchi zinawajibika kwa Sherika za kimataifa

Akijibu swali kuhusu ripoti kwamba UNIFIL kushambuliwa na Jeshi la Ulinzi la Israel jana Alhamisi, Bi. Shamdasani amesisitiza kuwa “mataifa yanalazimika chini ya sheria za kimataifa kuhakikisha kwamba walinda amani hawashambuliwi na , kwamba wanalindwa".

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wako kusini mwa Lebanon kuunga mkono kurejea kwa utulivu chini ya mamlaka ya azimio la Baraza la Usalama la 2006. Shambulio lolote la makusudi dhidi ya walinda amani ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama, UNIFIL imesema katika taarifa yake kufuatia tukio hilo, huku kukiwa na uharibifu mkubwa wa IDF wa miji na vijiji kusini mwa Lebanon, na mashambulizi ya makombora yanayoendelea kaskazini mwa Israel.

Bi. Shamdasani amesema. "Tarehe 9 na 10 Oktoba, Hezbollah ilisema imerusha angalau makombora 360 kutoka kusini mwa Lebanon hadi Israel.Watu wawili waliuawa katika shambulio la roketi kwenye mji wa mpakani wa Kiryat Shmona tarehe 9 Oktoba, siku moja baada ya wengine watano kujeruhiwa katika shambulio la roketi huko Haifa."

UNICEF WFP wanaendelea kutoa msaada muhimu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF na la mpango wa chakula duniani WFP yamesema licha ya hangamoto zinazoendelea za kiusalama nchini Lebanon jana yamesafiri hadi Rmeich kwenye mpaka wa Kusini wa nchi hiyo ili kutoa msaada muhimu kwa maelfu ya familia.

Kupitia mtandao wa kijamii wa X mashirika hayo yamesema  wakipeleka msaada huo muhimu wamepita na kushuhudia uharibifu  mkubwa wa miji na miundombinu kutokana na makombora ya Israel.

Miongoni mwa vifaa muhimu walivyogawa kwa familia ni Pamoja na vifaa vya usafi na kujisafi, maji na chakula.

Mashirika hayo yamesisitiza kuwa “Tuko hapa tunafanyakazi bila kuchoka ili kutoa msaada muhimu wa kuokoa maisha na huduma , na licha ya changamoto tutaendelea kufanya hivyo.”

Mashirika hayo yamesema pia yametuma msafara wa pili wa misaada ya kibinadamu kutoka Beirut hadi Rmaych, mojawapo ya maeneo yaliyoathirika zaidi hivi karibuni.

Source : UN Habari

SHARE THIS POST