Ulimwenguni kote, nchi 67 bado zinaharamisha uhusiano wa jinsia moja, huku 10 zikitoa hukumu ya kifo.

26 Julai 2024 Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu (OHCHR) leo imeelezea makubwa kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu ya Ghana kuunga mkono vifungu vya Sheria vinavyoharamisha uhusiano baina ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Akizungumza na vyombo vya habari kutoka Geneva, Uswisi, msemaji wa OHCHR Liz Throssell, ameelezea wasiwasi wake kuhusu uamuzi huu uliotolewa tarehe 24 Julai, hasa zikizingatiwa ripoti za ongezeko la uhasama dhidi ya watu wa wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja  LGBTQ+  nchini Ghana.

Amevitaja vifungu hivyo vya sheria ni kama vile vya “enzi za ukoloni”, akibainisha kwamba ingawa mswada wa haki za kijamii na maadili ya familia bado unakabiliwa na changamoto za kisheria, haujapata kibali cha rais licha ya kupitishwa na Bunge mwezi Februari 2024.

Liz Throssell amesisitiza maoni ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk, kwamba muswada huu unaoitwa "muswada wa uhusiano wa jinsia moja" wa 2024 ni wenye madhara makubwa.

Ameonya kuwa unahalalisha ubaguzi katika jamii na kuwaweka watu kwenye hatari ya ubaguzi, ukiukwaji wa haki ya faragha, uhalifu wa chuki na uhasama.

Mswada unachochea ubaguzi

Throssell ameongeza kuwa  muswada huu unapanua wigo wa nafasi ya ubaguzi usiozingatia sheria dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja  LGBTQ+   na pia unaharamisha kazi za watetezi wa haki za binadamu, wataalamu wa matibabu, walimu, wapangaji wa nyumba, waandishi na  wafanyakazi wa vyombo vya habari.

Throssell ametoa wito kwa serikali ya Ghana kutekeleza wajibu wake chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mikataba ya haki za binadamu ambayo imeiridhia, na kuhakikisha kuwa watu wote wanaoishi Ghana, bila ubaguzi, wanaweza kuishi bila uhasama, unyanyapaa na ubaguzi.