Marafiki watatu katika eneo la Afar nchini Ethiopia ambao wanapigania haki za wasichana na hatua dhidi ya ukeketaji wa wanawake (FGM) na ukatili wa kijinsia.
11 Oktoba 2024 Haki za binadamu
Ikiwa le oni Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa kuwapa sikio watoto wa kike akianza ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii akisema uwezo wa wasichana zaidi ya bilioni 1.1 duniani hauna kikomo lakini tunapokaribia tarehe mwaka 2030, wa mwisho kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu, ulimwengu unaendelea kuwaangusha wasichana.
“Wasichana wanachangia zaidi ya asilimia 70 ya maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi, VVU” anasema Guterres na kwamba wana uwezekano mara mbili zaidi wa wavulana kukosa elimu au mafunzo. Na ndoa za utotoni bado zimeenea, huku takriban msichana mmoja kati ya watano duniani akiolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Kotekote duniani, mafanikio yaliyopatikana kwa bidii ya usawa wa kijinsia yanafutwa na vita dhidi ya haki za kimsingi za wanawake na wasichana, na kuhatarisha maisha yao. kuzuia uchaguzi wao, na kuweka kikwazo cha mustakabali wa wasichana.
Wanawake waandamana kupinga unyanyasaji wa kijinsia nchini Ecuador.
Kwa kutumia kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambayo ni ‘Dira ya Msichana’ kwa Zama Zijazo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, wasichana tayari wana dira ya ulimwengu ambamo wanaweza kustawi. Wanafanya kazi kugeuza maono hayo kuwa vitendo, na kutaka sauti zao zisikike. Ni wakati muafaka sisi kusikiliza. Ni lazima tuwape wasichana nafasi kwenye meza, kupitia elimu, na kwa kuwapa rasilimali wanazohitaji na fursa za kushiriki na kuongoza.
Ujasiri, matumaini na uamuzi wa wasichana ni nguvu ya kuzingatia. Ni wakati wa ulimwengu kuchukua hatua na kusaidia kubadilisha maono na matarajio yao kuwa ukweli.