Nchimbi kukipeleka kikokotoo kwa Rais

7 months ago 986

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, ameahidi kufikisha kilio cha kikokotoo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, huku Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Abdulrahman Kinana akiwatahadharisha wananchama wa chama hicho kuwa, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani utakuwa wa ushindani na kuwataka wasibweteke.

Viongozi hao walitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti wakiwa katika mwendelezo wa ziara zao mkoani Rukwa na Mara.

Akiwa mkoani Rukwa, Dk. Nchimbi amewaahidi wastaafu na watumishi waliopo kazini kwamba atawasilisha kero ya kikokotoo kwa Rais Samia kwa ajili ya utatuzi, akisisitiza imekuwa kero kubwa kwa wastaafu.

Dk. Nchimbi amesema: “Tatizo la kikokotoo linalalamikiwa sana na watumishi, imekuwa kero kubwa, kuna muda lazima tuangalie wananchi wetu, wanachama wetu, tuangalie tutafika wapi, lakini kwa kadri inavyowezekana tunapaswa kutatua kero za wananchi.”

Ameongeza: "Nitalifikisha suala hilo katika uongozi wa juu kuona namna ya kulitafutia ufumbuzi kwakuwa lengo la CCM ni kutatua kero za wananchi."

Pamoja na mambo mengine, Dk. Nchimbi amewataka waliopewa zabuni ya kujenga Uwanja wa Ndege wa Rukwa kuongeza kasi ili kuendana na matakwa ya mkataba.

Amewataka viongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), mradi huo unajengwa kwa ubora, akiwahimiza kutanguliza uzalendo kwa maslahi ya taifa.

Amesema kwa mujibu wa mkataba uwanja huo unapaswa kukamilika ndani ya miezi 18, lakini mpaka sasa ni asilimia nane pekee zimekamilika.

Pia, ameahidi kuwasiliana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kutatua tatizo la uhaba wa madaktari bingwa mkoani Rukwa.

Kadhalika, amewataka wanachama wa CCM kuchagua viongozi wenye sifa, huku akisistiza katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa.

Akijibu hoja ya mmoja wa wananchama wa CCM ameyetaka mabalozi wa shina wa chama hicho walipwe mshahara, Dk. Nchimbi alisema suala hilo haliwezekani kwa sababu wao ndiyo wenye chama.

Hata hivyo, amesema mazingira yatakaporuhusu watapewa kifuta jasho na wasipopata wajue hali ya chama sio nzuri.

Naye Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla, alipokea kero 57 na kuagiza uongozi wa mkoa kuzipitia na kumrejeshea majibu.

Katibu wa NEC Oganaizesheni CCM, Issa Gavu, amewataka viongozi walioko ndani ya chama kujituma kwa kuwatumikia wananchi sambamba na kujenga utamaduni wa kusikiliza kero zao.

Pia, amewataka wajumbe wa mashina ya CCM kujenga utamaduni wa kukaa vikao vya kila mwisho wa mwezi na kwamba hilo litaleta chachu ngazi ya tawi kutimiza majukumu yao.

UCHAGUZI

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana akiwa mkoani Mara amewaonya wanachama wa chama hicho kutobweteka, kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwakani utakuwa mgumu.

Akizungumza jana katika kikao cha wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, amesisitiza kufuatwa kwa maadili ya uchaguzi.

“Zile sheria za uchaguzi zilizotungwa bungeni zinatoa nafasi ya ushindani, kwa hiyo msibweteke, badala yake tujipange vizuri. Tunatakiwa tujipange wanachama ili tupate ushindi wa kishindo mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025,” amesema Kinana.

Amesema kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni vema wana CCM wakashikamana na endapo kuna mtu mchana yuko upande wa CCM na usiku upinzani anapaswa kuwekwa kando haraka.

Kuhusu viongozi walioko madarakani wakiwamo madiwani na wabunge, Kinana alisema waachwe wafanye kazi akieleza kuwa hakuna sababu ya kuwavuruga kwa sababu kipindi cha uchaguzi bado hakijafika.

Pia, amekemea tabia ya ukabila akisema ni mambo ya kizamani na yanawagawa.

Kinana amesema nchi kuwa na makabila ni jambo la kawaida ila ukabila ni jambo baya.

Amesema Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere alitoka Mkoa wa Mara moja ya kabila dogo na ameongoza nchi kwa miaka 24, alipendwa, aliheshimiwa, alithaminiwa na alitukuzwa sio kwa sababu ya ukabila bali ni kazi aliyokuwa anafanya, utendaji na uadilifu wake uliomfanya aheshimike Tanzania, Afrika na duniani.

Source : Kimataifa

SHARE THIS POST