Kwa mujibu wa DMT zaidi ya watu milioni 10 wamelazimika kukimbia makazi yao – watu milioni 7.9 wamekimbia kutafuta usalama mahali pengine nchini humo, na zaidi ya watu milioni 2.2 wamevuka mipaka kusaka hifadhi katika nchi nyingine.
Wahamiaji na wakimbizi kutoka Sudan wanaongezeko la wasiwasi wa ulinzi, hasa katika nchi za Ethiopia na Kusini.
Timu za DTM zilizopo mashinani pia zimebainisha uwezekano wa watu kuhama kutokana na mafuriko wakati wa msimu ujao wa mvua kati ya mwezi Julai na Septemba 2024. Mvua hizo huenda zikaongeza changamoto za kuwafikia wenye uhitaji sio tu nchini Sudan bali pia katika nchi za ukanda huo zikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad, ambazo tayari zimeshashuhudia uharibifu wa makazi na barabara kutokana na mvua.
Katika nchi jirani ya Libya, IOM ilikutana na Balozi wa Sudan nchini Libya kuthibitisha uungwaji mkono kamili kwa Wasudan walio katika mazingira magumu walioathiriwa na mzozo.
Zaidi ya asilimia 97 ya wakimbizi wa ndani kote nchini Sudan wako katika maeneo yenye viwango vya juu vya uhaba wa chakula au hali mbaya zaidi (IPC level 3+), hii inajumuisha katika maeneo ambayo ni magumu kufikiwa kama vile Darfur. Kusaidia watu wote wenye uhitaji kunategemea ufikiaji salama na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu, usio na vikwazo vya urasimu, kwa njia zote.
Kwa mwaka huu wa 2024, IOM imefanikiwa kufikia jumla ya watu 1,177,953 hadi sasa kupitia usaidizi wa sekta mbalimbali. Licha ya mafanikio makubwa katika nchi ya Sudan na nchi jirani, mapengo makubwa yanasalia katika kuongeza operesheni ya kikanda za kibinadamu.
Mpaka sasa IOM imepata ufadhili wa asilimia 21 pekee ikiwa tayari tupo katikati ya mwaka, na hivyo kunahitajika fedha zaidi ili kuongeza shughuli na kufikia vipaumbele kote kanda na kuwasaidia wenye uhitaji.
Pamoja na uhaba huo wa fedha lakini IOM inaendelea kutoa msaada wa kibinadamu unaohitajika sana nchini Sudan na katika nchi jirani, huku ikitetea upatikanaji salama na usiozuiliwa wa misaada kwa watu walioathirika zaidi.
Wakimbizi wa Sudan wakusanyika kwenye kivuko cha Joda kwenye mpaka wa Sudan Kusini.
Hivi ndivyo IOM ilivyosaidia katika nchi mbalimbali
• Nchini Sudan, IOM ilianzisha kliniki inayotembea huko Gedaref, pamoja na washirika wa ndani, ili kutoa usaidizi wa kimatibabu kwa idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani wanawaowasili kutoka jimbo la Sennar.
• Nchini Chad, kaya 5,131 zilizorejea nchini mwao kutoka ukimbizini nchini Suan zilipokea maturubai katika mkoa wa Ouaddaï ili kupata makazi na kujilinda na mvua zinazoendelea kunyesha.
• Nchini Sudan Kusini, watu 9,612 walisaidiwa kupewa usafiri wa kuendelea kuelekea wanapotaka - watu 5,852 walisafirishwa kwa barabara, watu 1,362 kwa boti, na watu 2,398 kwa ndege.
• Nchini Ethiopia, watu 493 waliorejea makwao kutoka ukimbizini walisafirishwa kutoka mahali pa kuingilia hadi katika Kituo cha kutoa msaada kwa Wahamiaji.
• Nchini Misri, Watu 60 walipokea huduma za afya, ikijumuisha uchunguzi wa afya, ushauri nasaha na dawa.
• Nchini Libya, wahamiaji 381 wa Sudan walisaidia kwa bidhaa zisizo za chakula kama vile nguo, vifaa vya usafi, magodoro, blanketi, seti za jikoni, na taa za jua, wakati wahamiaji 75 wa Sudan walipokea vifurushi vya chakula ndani ya eneo la Tripoli.