Shirika la misaada ya matibabu MSF linasema kuwa linalazimika kusitisha kazi zake katika kambi kubwa ya watu wasiokuwa na makazi ndani ya nchi ambako njaa imethibitishwa katika mkoa wa North Darfur nchini Sudan na kusababisha maelfu ya watoto walio na utapiamlo kuwa katika hatari ya kifo.
MSF imesema ililazimika kusitisha shughuli zake katika kambi ya Zamzam kufuatia kuingiliwa kwa shughuli ya misaada karibu na al-Fashir zinazofanywa na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), ambao wamekuwa wakiuzingira mji huo kwa miezi kadhaa, pamoja na utaratibu wa jeshi la Sudan unaozuia misaada kwenda maeneo wanayoyadhibiti.
Jeshi na RSF wamekuwa katika mgogoro kwa karibu miezi 18, hali iliyosababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambapo zaidi ya watu milioni 10 wamelazimika kuondoka majumbani mwao, na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanataabika kusambaza misaada.