Rosine mwenye umri wa miaka 15 akiwa amemshikilia mpwa wake mchanga ndani ya chumba cha matibabu cha mpox kinachoungwa mkono na UNICEF katika Hospitali ya Kavumu katika jimbo la Kivu Kusini, DR Congo, tarehe 14 Septemba 2024.
9 Oktoba 2024 Afya
Ukisikia makovu yasiyofutika ni ya simulizi hii utakayoisikia kuhusu familia moja huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kupoteza watoto wanne kutokana na ugonjwa wa homa ya nyani au mpox huku mustakabali wao ukisalia mashakani kwani bado hawafahamu hali itakuwa vipi kwenye familia yao, baba na mama wakipambana na ugonjwa huo.
Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyochapishwa kwenye mtandao wa Instagram unatupeleka Mbandaka, mji ulioko jimboni Equateur, kaskazini-magharibi mwa DRC.
Dkt. Douglas Noble Mkurugenzi Mshiriki, UNICEF ndiye mwenyeji wetu hapa kwani ametembelea kituo cha matibabu ya mpox hapa Mbandaka na anasema, “tuko hapa Mbandaka, ambapo kuna idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa mpox. Tumetembelea kituo cha matibabu, na ni huzuni kusikia hadithi ya familia moja yenye watoto sita, ambapo wanne walifariki dunia kwa mpox. Watoto wawili wako vizuri kwenye kituo cha watoto. Baba na mama bado wako kituo cha matibabu."
Ni kwa kuzingatia madhara ya ugonjwa wa mpox kwa watoto na jamii nchini DRC ndio maana Dkt. Noble anasema “simulizi kama hizi zinatufanya tutambue uzito wa ugonjwa huu kwa watoto na jinsi unavyoathiri jamii. Wito wetu ni kuwahamasisha watu na kujenga uwezo wao ili waweze kudhibiti hali hii.”
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC inatajwa kubeba asilimia 90 ya wagonjwa wote 18,815 walioripotiwa duniani kote.