MNEC Simiyu awapa mbinu ya kiutendaji wabunge, madiwani

7 months ago 971

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Gungu Silanga.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Gungu Silanga amewapa mbinu za kiutendaji madiwani na wabunge ambazo zitawasaidia kutoyumbishwa wakati wakitekeleza majukumu yao kulingana na nafasi zao.

Akizungumza leo Wilayani Bunda, mkoani Mara, wakati wa kikao cha ndani cha wanachama wa CCM, MNEC Silanga, amewaeleza viongozi hao kwamba mbinu pekee ya kuhakikisha wanaimarisha ufanisi wao katika utendaji ni kuacha kusikiliza au kuwa na mashaka na watu wanaopiga kelele kwa lengo la kuwavuruga.

Pia amewasisitiza wabunge na madiwani kuhakikisha kwamba wanaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na uadilifu kwakuwa wananchi wanaona na kuridhishwa na utekelezaji wa ilani ya chama hicho katika kuwaletea wananchi maendeleo.

"Wana Bunda kwanza nawapongeza kwa ushindi ambao mumeupata mwaka 2020 kwa kupata madiwani na wabunge wengi. Watu wa Bunda wako timamu na sidhani kama kutakuwa na shida yoyote, pia ni wachapakazi, wapambanaji na mfumo wa chama chetu ni kufanya kazi kwa uwazi na ukweli.

“Madiwani na viongozi wengine fanyeni kazi ya kutekeleza llani ya 2020, wanaopita na kupiga kelele achaneni nao, ukifanya kazi wananchi na wana CCM wanaona. Fanyeni kazi chama kipo imara, Rais Samia Suluhu Hassan yuko imara na kamati ya siasa wilaya ya Bunda inafanya kazi,” amesema Silanga.

Pia amewahimiza wana CCM kuendelea kushikamana, akieleza kwamba chama hicho ili  kiendelee kushika dola ni pale ambako muungano na mshikamano utaendelea kuimarishwa.

Silanga ni miongoni mwa WaNEC ambao wameongozana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Abdulrahman Kinana ambaye yuko kwenye ziara katika wilaya hiyo akitokea Serengeti. Rorya, Tarime na Butiama.

Source : Kimataifa

SHARE THIS POST