Mlandege yaona mwezi Zanzibar

2 months ago 22

By  Mwandishi Wetu

Mwananchi Communications Limited

MABINGWA wa Kombe la Mapinduzi 2024, Mlandege jana imeonja ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu Zanzibar kwa msimu huu baada ya kuinyoa Mafunzo kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan kwa Wazee mjini Unguja.

Mlandege iliyotwaa taji la Mapinduzi mapema mwaka huu kwa kuifunga Simba kwa bao 1-0 katika fainali kali iliyopigwa Januari 13 kwenye Uwanja wa New Amaan, huo ulikuwa ni mchezo wa tatu kwao katika ligi kama ilivyo kwa maafande wa Mafunzo ambao wanapoteza kwa mara ya kwanza msimu huu.

Bao lililowazamisha Mafunzo na kuipa Mlandege ushindi wa kwanza liliwekwa kimiani na Rafael Charles Futakamba dakika ya 61 kwa penalti na kuifanya timu hiyo sasa kufikisha pointi tano kwani awali ilitoka suluhu mbili mfululizo dhidi ya Chipukizi na Junguni zote za Pemba.

Pointi hizo zimeitoa nafasi ya 12 iliyokuwapo hadi ya sita, wakati Mafunzo imeporomoka kwa nafasi mbili kutoka ya pili hadi ya nne ikisaliwa na pointi sita.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Annex A, wageni wa ligi hiyo, Inter Zanzibar iliendelea kutoa takrima kwa kufumuliwa mabao 2-1 na Uhamiaji iliyochupa kutoka nafasi ya tisa hadi ya pili kwa kufikisha pointi sita na mabao matano ya kufunga na kufungwa manne.

Katika mechi hiyo iliyokuwa kali, Inter Zanzibar iliyopanda daraja msimu huu sambamba na Junguni, Mwembe Makumbi na Tekeleza, iliwabana maafande hao wa Uhamiaji na kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa kwa kufunga bao 1-1.

Uhamiaji ilikuwa ya kwanza kuandika bao dakika ya sita tu ya mchezo kupitia Daudi Goodluck Sovela, kabla ya Mudrik Miraji Mawia kulichomoa dakika ya 24, hata hivyo kipindi cha pili kilipoanza Inter ilishindwa kushikilia bomba vizuri kwa kuruhusu bao la pili dakika ya 72 kupitia Abel Simwinga Mathias.

Matokeo hayo yamezidi kuifanya Inter kusalia mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa haina pointi hata moja kama ilivyo kwa Zimamoro na New City (ambayo jana ilikuwa uwanjani kuvaana na Malindi), zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa. Inter iliyocheza mechi tatu imefunga mabao mawili tu na kufungwa tisa.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST