Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya uenyekiti na rais wa Heshima, Mohammed Dewji ‘MO’ ilieleza kwamba Regis ataanza kazi Agosti Mosi, mwaka huu, baada ya Kajula kumaliza mkataba wake.
KLABU ya Simba juzi ilimtambulisha, Uwayezu Francois Regis, raia wa Rwanda kuwa ofisa mtendaji mkuu (CEO), akirithi mikoba ya Imani Kajula.
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya Mwenyekiti na rais wa Heshima, Mohammed Dewji ‘MO’ ilieleza kwamba Regis ataanza kazi Agosti Mosi, mwaka huu, baada ya Kajula kumaliza mkataba wake.
Mojawapo wa mambo makubwa yatakayombeba Regis ni uzoefu alionao katika soka la Afrika, kwani kabla ya hapo alikuwa makamu mwenyekiti wa APR ya Rwanda, huku akiwahi pia kuwa katibu mkuu wa Chama cha Soka Rwanda (Ferwafa).
Wasifu wa Regis unaonyesha ana uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika uongozi wa michezo na hasa soka, ambapo anakumbukwa pia kuwa miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha Makocha wa sSoka Rwanda ambacho amewahi kuwa makamu wa rais.
Regis pia ana taaluma ya ukocha wa soka akiwa na leseni ngazi B ya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (Uefa) aliyoipata Ujerumani.
Regis ni mtaalamu wa masuala ya utawala wa biashara akiwa na elimu ya ngazi ya shahada ya uzamili huku akiwa ana cheti cha kimataifa cha utunzaji wa fedha za umma (IPSAS), na wakati huohuo aliwahi kufanya kazi kama mkaguzi mkuu wa ndani wa Rwanda.
Mbali na hilo, lakini amekuwa mkurugenzi wa utawala na fedha na mkurugenzi wa uendeshaji wa taasisi tofauti ndani ya Rwanda, jambo ambalo halitakuwa shida kwake kuiongoza timu hiyo licha ya kuwepo kwa mazingira tofauti ya kiuendeshaji.
Regis anakuwa mtendaji wa pili wa Simba kutoka nje ya nchi kwani awali ilimuajiri Senzo Mazingisa kutoka Afrika Kusini ambaye baadaye alijiondoa na kujiunga na Yanga kabla ya kurithiwa na Mzambia Andre Mtine aliyetokea TP Mazembe ya DR Congo.
Wakati Simba ikitangaza kumuajiri Regis, Mwanaspoti linakuletea mambo yanayomkabili bosi huyo mpya.
MATAJI
Moja ya mitihani mikubwa anayokabiliwa nayo Regis ni kurejesha heshima ya klabu hiyo kwa kutwaa mataji hususan Ligi Kuu Bara ambayo kwa misimu mitatu mfululizo Simba imeshuhudia yakienda kwa wapinzani wa jadi, Yanga.
Simba mara ya mwisho kutwaa taji la Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu wa 2020-2021, chini ya aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez aliyetangaza kujiuzulu Desemba 10, 2021 na nafasi yake kuchukuliwa na Kajula, Januari 26, 2022.
Ndani ya misimu mitatu chini ya Kajula, Simba imeshinda taji moja la Ngao ya Jamii mbele ya watani zao, Yanga ambao walikuwa chini ya kocha mwenye uraia wa Tunisia na Ubelgiji, Nasreddine Nabi ambaye kwa sasa anainoa Kaizer Chiefs ya Sauzi.
Simba iliyosajili kwa kiasi kikubwa wachezaji wengi msimu huu huku ikiwa na benchi jipya la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, imedhamiria kurejesha heshima yake msimu ujao japokuwa haitakuwa rahisi kutokana na wapinzani pia kujipanga kuendeleza ubabe.
TIMUA TIMUA MAKOCHA
Katika uongozi wa Kajula ambaye anaondoka akiwa hana rekodi za kuipa mataji makubwa timu hiyo, alishatimua makocha watano katika muda aliokalia kiti hicho, huku wageni wakiwa wanne na mzawa mmoja - Juma Mgunda.
Makocha wageni ni Pablo Franco aliyetua Simba akahudumu kwa miezi sita kabla ya Mei 2022 kutimka na nafasi yake kuchukuliwa na Zoran Maki, Juni 22 na kuondoka Septemba 22 akiwa ni kocha aliyedumu kwa muda mfupi zaidi Msimbazi.
Septemba 2022, mzawa Mgunda alipata nafasi ya kuifundisha Simba akihudumu kwa miezi mitano na kujiwekea rekodi ya kuiongoza timu hiyo kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa ni mzawa wa pili baada ya Tito Mwaluvanda wa Yanga 1998 kufanya hivyo.
Mgunda aliiongoza Simba katika michezo 18 na kati ya hiyo alipoteza mmoja ingawa pia aliondolewa ilipofika Januari 3, 2023.
Baada ya hapo Simba ilimtambulisha Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyeiongoza katika michezo 12 akishinda saba, sare nne na kupoteza mmoja dhidi ya Yanga kwa mabao 5-1 na hapo ndipo ikawa safari yake ya mwisho.
Kuondoka kwa Robertinho Novemba 7, 2023 kuliifanya Simba imtambulishe Mualgeria Abdelhak Benchikha Novemba 24, 2023, ingawa alidumu kwa siku 156 na akaondoka Aprili 28, 2024, kwa kile kilichoelezwa kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.
Benchikha aliondoka ndani ya kikosi hicho ikiwa ni siku moja tu tangu aipe taji la Kombe la Muungano lililohitimishwa Aprili 27, 2024 Zanzibar baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.
Baada ya hapo Julai 5, 2024, Simba ilimtangaza Kocha Fadlu Davids, raia wa Afrika Kusini ili kuchukua mikoba ya Benchikha ikiwa ni muda mfupi tangu aipe ubingwa wa Ligi Kuu Morocco timu ya Raja Casablanca akiwa msaidizi wa Josef Zinnbauer.
Huu ni mtihani mwingine ambao Regis anaokwenda kukabiliana nao ndani ya kikosi hicho kwani licha ya timu hiyo kusifika kwa rekodi nzuri kimataifa, lakini imekuwa haidumu na makocha na kuthibitisha hilo tayari imeshatimua tisa ndani ya misimu sita.
KIPIGO CHA WATANI
Regis anatua Simba huku akikumbana na mtihani wa kwanza mzito wakati kikosi hicho kitakapokutana na wapinzani na Yanga, katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba inaingia katika mchezo huo wa Dabi ya Kariakoo huku ikiwa na kumbukumbu mbaya kwani msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara ilipoteza michezo yote miwili ikianza na kichapo cha mabao 5-1, kisha mzunguko wa pili ikachapwa 2-1.
Hata hivyo, timu hiyo ina kumbukumbu nzuri dhidi ya Yanga kwani mara ya mwisho zilipokutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ulipigwa Agosti 13, 2023, ilishinda kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya kushindwa kutotambiana ndani ya dakika 90.
NUSU FAINALI CAF
Shauku kubwa ya Simba ni kufika nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya misimu ya karibuni kuishia robo fainali jambo ambalo Regis anaingia madarakani huku akikabiliwa nalo mbeleni, ingawa msimu huu inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika malengo ni yaleyale. Simba imefika robo fainali tano ndani ya misimu sita katika michuano ya CAF tangu 2018-19 zikiwemo nne za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho na mara zote imekwamia hapo.
Msimu huu itashiriki Kombe la Shirikisho baada ya kumaliza nafasi ya tatu msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga na Azam zilizokata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini itaanza kucheza katika hatua ya pili.
Timu hiyo itasubiri mshindi wa jumla kati ya Libya 1 ya Libya dhidi ya wawakilishi wengine wa Tanzania kutoka Zanzibar, Uhamiaji huku ikionekana huenda ikafanya vizuri zaidi kutokana na timu shiriki msimu huu.
KUKUZA UDHAMINI
Katika suala la udhamini hakuna shida sana Simba kwani imekuwa ikiingia mikataba mingi na kampuni tofauti za ndani na nje ya nchi japokuwa Regis anapaswa kuhakikisha anaendelea kutengeneza ushawishi kwa kampuni zingine.
Suala hilo litafanikiwa tu endapo timu hiyo itaendelea kufanya vizuri ndani na nje ya nchi kwa sababu klabu nyingi huwa zinapata udhamini kutokana na mafanikio zinayopata, kwa sababu wawekezaji wanaamini hiyo ndio fursa ya kutangaza biashara zao.
MIUNDOMBINU
Katika mikakati ya kusuka upya kikosi ndani na nje ili kupata matokeo chanya, Regis anakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha kinakuwa na miundombinu bora itakayorahisisha kazi kwa wachezaji na benchi la ufundi. Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa viwanja bora vya kufanyia mazoezi na hata michezo ya timu ya wanawake ya Simba Queens imekuwa ikichezewa hapo, ingawa bado haukidhi vigezo vya kimataifa.
SOKA LA VIJANA
Simba ni miongoni mwa timu ambazo miaka ya nyuma zilikuwa zikisifika kwa kukuza soka la vijana kwani baadhi walitokea huko na kupandishwa kwa wakubwa japokuwa kwa sasa hali imebadilika na imekuwa ikitumia gharama kubwa kusajili mastaa nje ya nchi.
Miongoni mwa nyota wanaokumbukwa walioanzia timu ya vijana Simba ‘B’ na kupandishwa ni kiungo Jonas Mkude aliyeitumikia kwa zaidi ya miaka 10 kisha akaondoka Julai 12, mwaka jana na kujiunga na Yanga.
MSIKIE MOGELLA
Akimzungumzia Regis, nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella anasema hana shaka naye kutokana na uzoefu mkubwa alionao kule alikotoka, japokuwa anapaswa kujiandaa kisaikolojia kwa sababu ya presha kubwa atakayokutana nayo.
“Ukiangalia wasifu wake kwa maana ya CV unaona ni mmoja wa viongozi wakubwa anayeonekana anatosha kuvaa viatu vya kuiongoza Simba ingawa wasiwasi wangu mkubwa ni jinsi atakayoweza kuendana na presha kubwa iliyopo nchini,” anasema Mogella.