Unguja. Matumizi sahihi ya mfumo wa kidijitali wa anuani za makazi (Napa) utapunguza urasimu, udanganyifu na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla, imeelezwa.
Hayo yamebainika wakati wa kukabidhi vifaa na uzinduzi wa majaribio ya kutoa huduma ya barua ya utambulisho wa ukaazi kupitia mfumo wa kidijitali wa anuani za makazi (Napa).
Akizungumza katika uzinduzi huo Julai 25, 2025 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Mngereza Mzee amesema mfumo huo una mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo utalii, kwani utakuwa ukionyesha huduma kadhaa zikiwamo hoteli na vivutio vilivyopo katika maeneo husika.
“Changamoto zitatatuliwa kupitia njia hii ya kidijitali ikiwemo kuondoa au kupunguza udanganyifu, msongamano katika ofisi za masheha na kupunguza muda wa kupata wahusika,” amesema.
Amesema mfumo huo utamwezesha mwananchi kuwa na barua ya utambulisho wa mkazi kupitia simu yake bila kulazimika kwenda kufuata barua hiyo kwenye ofisi za sheha au Serikali kama ilivyo sasa.
Vifa vilivyogawia ni kompyuta za mezani, printa na vishikwambi ambavyo vitatumiwa na masheha kutoa huduma za barua za makazi.
Amesema wizara itahakikisha vishikwambi vinavyogawiwa vinakuwa na intaneti hivyo watendaji hawataingia gharama za ununuzi wa bando katika kipindi chote cha majaribio cha miezi mitatu.
Dk Mngereza amesema kuanzia kipindi cha operesheni za anuani za makazi mwaka 2022 hadi sasa jumla ya anuani 495,223 zimekusanywa na kuhifadhiwa katika mfumo huo wa Napa.
Mratibu msaidizi wa utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi kitaifa, Mkude Arnold amesema baada ya kufanya operesheni za anuani za makazi mwaka 2022 walikusanya taarifa 12.8 milioni zilizopo kwenye mfumo.
“Taarifa hizi lengo la Serikali ni zitumike katika kuboresha huduma na miongoni mwa hizo ni kutoa barua za utambulisho. Tunafahamu utaratibu wa sasa mwananchi anakwenda kwa mwenyekiti wa mtaa au sheha ili kupata barua ya utambulisho sasa imedhamiriwa kuondolewa,” amesema.
Amesema baada ya kufanya majaribio katika shehia hizo nne watakwenda nchi nzima kwa hiyo kila mwananchi anatakiwa kujua anauni zake za makazi, ajue namba yake ya nyumba, jina la barabara na namba maalumu ya kata ambavyo ni vitu vya msingi kufahamu.
Baadhi ya masheha na wasaidizi wao wamesema mfumo huo utawapunguzia kazi.
Fatma Abdallah Abdi, mjumbe wa shehia ya Gulioni amesema wamepata mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo huo, kwa hiyo watahakikisha wanakwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.