Mfanyakazi wa misaada wa Gaza aliyerekodi kwa simu kifo chake - BBC News Swahili

1 day ago 56

Mfanyakazi wa misaada wa Gaza aliyerekodi kwa simu kifo chake

a

"Moyo wangu na roho yangu vilienda na Rifaat," anasema Haja Umm Muhammad, mama wa mmoja wa wafanyakazi wa misaada wa Kipalestina 15 waliouawa katika shambulio hatari lililofanywa na Israel dhidi ya msafara wao.

Mnamo Machi 23, Rifaat Radwan mwenye umri wa miaka 23 alikuwa akisafiri ndani ya gari la wagonjwa la Jumuiya ya Msalaba Mwekundu ya Palestina akiwa pamoja na msafara wa magari ya dharura wakati waliposhambuliwa kwa risasi.

"Sikuwahi kufikiria kuwa atauawa," anasema mama yake Rifaat. "Haswa kwa sababu eneo hilo linajulikana kama eneo la kijani. Hiyo inamaanisha ni eneo salama na magari ya wagonjwa yanaruhusiwa kupita."

Israel ilidai awali kwamba wanajeshi wake walifyatua risasi dhidi ya msafara " walioutilia shaka" wa magari kadhaa na uliokuwa ukielekea kwenye eneo lao usiku. Hata hivyo, video aliyopiga Rifaat muda mfupi kabla ya kuuawa, ambayo ilipatikana kwenye simu yake baada ya kifo chake, inaonesha taa za magari ya msafara zilikuwa zimewashwa, na walikuwa wakienda kutoa msaada.

Katika video hiyo, kabla ya kuuawa, Rifaat anasikika akisema kwa sauti yake:

"Nisamehe mama, hii ndiyo njia niliyochagua kusaidia watu..."

Umm Muhammad anasema kuwa kwa kusema hivyo, Rifaat alikuwa anamuomba msamaha kwa sababu alijua hataweza kumwona tena.

"Kila mara Rifaat alipokwenda kazini, nilikuwa namuombea kwa Mungu," anasema. "Alikuwa jasiri na alisafiri kote Gaza, kutoka kaskazini hadi kusini."

Rifaat alikuwa akifanya kazi kwa hiari na Jumuiya ya Msalaba Mwekundu ya Palestina baada ya shambulio lisilo la kawaida la Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 na kuanza kwa operesheni ya kijeshi ya Israel Gaza.

Umm Muhammad anasema mtoto wake alipenda shughuli za kibinadamu, kusaidia watu.

"Rifaat pia alikuwa akihusika katika kuwapeleka majeruhi hadi nchini Misri kupitia mpaka wa Rafah."

Anasema siku ambayo Rifaat aliuawa, walikuwa wameelekezwa kuwasaidia waathiriwa wa mashambulizi kadhaa yaliyosababisha vifo.

"Sikufikiria kama angekuwa miongoni mwa waliouawa," anasema.

Ilichukua wiki moja hadi mwili wake na ya wenzake ilipopatikana tarehe 30 Machi.

"Badala ya kusherehekea Eid al-Fitr, tulilazimika kwenda kwenye Shirika la Msalaba Mwekundu kuuchukua mwili wake kutoka Hospitali ya Nasser huko Khan Yunis na kumzika," anasema Umm Muhammad. "Mwili wake ulikuwa umeharibika sana kiasi kwamba hawakunikubalia kumuona."

Umm Muhammad anasema Rifaat alikuwa mtu "wa heshima ya kweli" na ndiye alikuwa mlezi wa familia baada ya ndugu zake wengine kuoa na kuolewa.

Baada ya kugundua video ya Rifaat, Israel ilikiri kuwa ripoti yao ya awali kwamba magari ya msafara yalikuwa hayana taa haikuwa sahihi, wakisema ripoti hiyo ilitolewa na wanajeshi waliokuwepo eneo hilo.

Afisa mmoja wa Israel alisema wanajeshi walizika miili ya wafanyakazi wa misaada 15, akiwemo Rifaat, kwenye mchanga ili kuwalinda dhidi ya wanyama wa porini. Miili hiyo haikugundulika hadi baada ya wiki moja kwa sababu mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa, yalishindwa kuratibu mazingira salama ya kuingia eneo hilo.

Wakati timu ya uokoaji ilipopata miili hiyo, simu ya Rifaat ambayo ilikuwa na video ya tukio hilo pia ilipatikana.

Jeshi la Israel liliahidi "kufanya uchunguzi wa kina" kuhusu tukio hilo na kusema linakusudia "kufafanua mlolongo mzima wa tukio hilo na jinsi lilivyoshughulikiwa."

Msalaba Mwekundu na mashirika mengi ya kimataifa wametoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu tukio hilo.

a
Maelezo ya picha, Munzer Abed, mfanyakazi pekee wa uokoaji aliyenusurika, anasema yeye na wenzake walishambuliwa na jeshi la Israel bila kupewa onyo lolote.

*"Nilianguka sakafuni nyuma ya gari la wagonjwa na sikuweza kusikia sauti yoyote kutoka kwa wenzangu isipokuwa pumzi zao za mwisho kabla ya kufa," anasema Munzer Abed, mfanyakazi pekee wa uokoaji aliyenusurika kwenye tukio hilo.

"Baada ya hapo, wanajeshi wa Israel walinikamata, wakaweka kichwa changu chini kwa nguvu, na kunizuia kuona kilichowapata wenzangu."

"Niliposikia wote wameuawa, nilivunjika moyo," anasema kwa huzuni. "Walikuwa familia yangu ya pili... ndugu zangu, marafiki zangu, vipenzi vyangu."

"Nilitamani ningekufa kwa hofu ya kile nilichokiona."

Anasema walipomkamata, pia walichukua simu yake.

"Walinichunguza kwa saa 15, wakinipiga, kunitukana, na kunitesa kimwili na kisaikolojia."

BBC imewasilisha simulizi ya Mundhar kwa jeshi la Israel, lakini hawajajibu bado.

Jumuiya ya Msalaba Mwekundu ya Palestina imesema eneo ambalo wafanyakazi wa misaada walikuwemo halikuwa limetangazwa kuwa "eneo jekundu" kwa maana ya eneo hatari na jeshi la Israel, na kwa hiyo hakukuwa na haja ya kufanya uratibu kabla ya kuingia.

Shirika hilo limesisitiza pia kuwa video hiyo inaonesha kuwa hakukuwa na magari ya kijeshi ya Israel yaliyoonekana kwenye eneo hilo.

Shirika hilo limeongeza kuwa ripoti za awali za uchunguzi wa kidaktari zinaonesha kuwa wahudumu hao waliuawa kwa "risasi nyingi sehemu za juu za miili yao," jambo linalothibitisha kuwa "walishambuliwa kwa makusudi."

Jumuiya ya Msalaba Mwekundu imekataa uchunguzi wa jeshi la Israel na pia imekanusha madai ya jeshi hilo kuwa wapiganaji wa Hamas walikuwemo miongoni mwa waliouawa, wakisema kuwa madai hayo hayakuambatanishwa na ushahidi wowote.

Jeshi la Israel lilitangaza kuwa Meja Jenerali Eyal Zamir, Mkuu wa Majeshi, alipokea matokeo ya awali ya uchunguzi huo na kuagiza uchunguzi huo kuendelezwa kwa kina zaidi na kukamilishwa katika siku chache zijazo, kwa mujibu wa utaratibu wa uchunguzi wa ndani wa jeshi hilo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa "madai yote yaliyotolewa kuhusu tukio hili yatachunguzwa kupitia utaratibu huu na kuwasilishwa kwa njia kamili na sahihi ili kuamua jinsi ya kushughulikia suala hilo."

Katika shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023, takribani watu 1,200 waliuawa na 251 kuchukuliwa mateka.

Tangu wakati huo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza, zaidi ya watu 50,800 wameuawa katika eneo hilo.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa Januari yalivunjika Machi, na hadi sasa mateka 58 bado wanashikiliwa Gaza, 24 kati yao wakiaminika kuwa hai.

Source : BBC Swahili

SHARE THIS POST