Mhariri wa jarida la burudani gazeti la Mwananchi
Mwanza. ‘Dhahabu ili ing’ae lazima ipite kwenye moto’ ni msemo ambao ameutumia Costasnia Kisege ambaye ni Mwalimu, Mwamuzi wa Mchezo wa Netiboli Ngazi ya Taifa, Mratibu wa Michezo Wilaya ya Maswa na Katibu Chama cha Mpira wa Netiboli Simiyu, wakati akielezea safari yake ya kuingia kwenye michezo.
Mama yake alipenda michezo baba yake hakupenda
Anasema licha ya kufanikiwa kwenye michezo, alipitia changamoto kutoka kwa wazazi wake kutomruhusu kutoka nje ya Mkoa kimichezo.
“Mimi kufanikiwa kwangu pia nimepita kwenye changamoto, kama wanavyosema dhahabu ili ing’ae lazima ipite kwenye moto. Nimelelewa kwenye familia ambayo iliniruhusu kucheza lakini siyo nje ya mkoa, nacheza naishia ndani ya wilaya.
“Mama yangu alipenda niingie kwenye michezo lakini baba yangu alikuwa hapendi nilikuwa naishia pale nilipokuwa naishia.”Amesema
Ameeleza kuwa baada ya kutoka mikononi mwa wazazi wake na kuanza kujitegemea alihakikisha anatimiza ndoto zake
“Baada ya hapo nilitoka mikononi mwa wazazi wangu, nililelewa na Mafinga JKT walitambua kipaji changu tangu nikiwa mtoto wakawa wameendelea kunitunza na kunikuza lakini baadaye nilipoenda kusoma nje nikawa nakwenda mikoani bila wazazi kutambua kwa sababu sikuwa mikononi mwao.
“Nilipoingia kazini tangu mwaka 1998, pale nilijipambania vizuri zaidi kwa sababu sikuwa chini ya wazazi tena nikaendelea na michezo nikasoma kozi mbalimbali huku nikiendelea kufundisha watoto”. Amesema
Kutokana na hayo amewataka watoto wenye vipaji kusimamia misimamo yao ili waweze kutimiza na kufikia malengo
“Watoto wasikate tamaa hata kama wakikatishwa na wazazi kuna njia nyingine ya kutokea, ukipata upenyo fanya kile unachohitaji kwa weledi hata kama upo shule ya bweni ama sehemu nyingine pembeni ya wazazi fanya kile unachokihitaji. ”. Amesema na kuongezea
“Mtoto wa kike anayetaka kufanikiwa kama mimi nilipofikia apende michezo kutoka moyoni, ukijua unataka nini katika maisha yako unaweza ukafikia malengo lakini pia kusapotiwa kutoka nje”. Amesema
Anavyonufaika na michezo
Michezo imeonekena kuwa na manufaa kwake katika kujipatia kipato na kuendesha maisha.
“Michezo ina fursa nyingi kama mimi hapa naenda kuendesha UMETASHUNTA kwa kufanya kazi hiyo sitoki bure wilaya inanilipa, pia napata fursa ya kufahamika na kupata marafiki.
“Nafahamiana na watu wengi kwenye nchi hii karibia kila mkoa kutokana na michezo ukiachilia mbali na kipato. Michezo inafanya afya yangu iwe imara siugui magonjwa ya kuamukiza.”Amesema
Changamoto kazini, amewataja matom boi
Kutokana na mitazamo ya baadhi ya watu kuwa mwanamke akiingia kwenye michezo hubadilika na kuiga tabia za kiume, Costansia amesema hicho ndicho kitu kikubwa anachokipiga marufuku.
“Kati ya vitu ambavyo navipiga marufuku nikimfundisha mtoto wa kike napenda aonekane wa kike moja kwa moja na si vinginevyo, japo kuwa wapo wengine wakifikia hatua hiyo ya kuanza kucheza soka wanaanza kujibadili na kuanzia mtembeo, mavazi, kutengeneza nywele yaani anaiga kitu cha mtu fulani maarufu kuliko kujitengeneza yeye.
“Mimi katika kukuza kwangu vipaji vya watoto hicho ni kitu ambacho huwa nakemea sana sipendi na haipendezi kama wewe ni mwanamke endelea kuwa mwanamke na utaonekana tengeneza jina lako wewe ufahamike wewe huwa sipendezwi na mtoto wa kike anayejiita Pakome, Mayele huwa nawaambia tengeneza jina lako ili tukutambue.”Anasema
Mbali na hiyo amesema ipo changamoto ambayo anakutana nayo kutoka kwa wazazi, ikiwemo kutokuamini katika michezo.
“Changamoto zipo nyingi za kimazingira, kiimani , kitamaduni lakini kwangu mimi nakutana nazo sana sana kutoka kwa wazazi na walezi, ukianza kumfundisha mtoto akifikia hatua fulani wazazi wengine wanaamini kuwa elimu ya darasani ni bora kuliko michezo unakuta mzazi au mlezi haamini katika michezo.
“Mara nyingi natumia muda kuwaelekeza kuwa michezo pia ni taaluma na wakati mwingine nawaambia mtoto anaweza kufanya vizuri kwenye michezo kuliko darasani”. Amesema na kuongezea
”Michezo yoyote siyo uhuni na wala siyo kuvunja taaluma kama mtoto wako anakipaji muache acheze inawezekana akaja kuwa mtu mkubwa kwenye jamii katika michezo kama wengine wanaofahamika
Wazazi wasiwakataze watoto wenye vipaji kucheza wawalete tuvikuze na watoto watimize ndoto zao inafika hatua mtoto anakuja kucheza mzazi anakuja uwanjani kumtoa na kusema hataki kumuona kwenye viwanja vya michezo”amesema
Ushiriki wa wanawake kwenye michezo
Licha ya kuwa yeye ni mmoja kati ya wanawake waliofanikiwa kuingia kwenye michezo anasema bado kuna tatizo kwani ushiriki wa wanawake ni mdogo mno.
“Ushiriki wa wanawake kwenye michezo si kwa asilimia kubwa hii inatokana na mazingira na tamaduni za baadhi ya mazingira kwani kuna wengine wanasema wanawake kushiriki kwenye michezo siyo heshima na haifai, asilimia kuwa watoto wa kike ni ngumu kushiriki michezo”. Amesema
Aidha amesema licha ya changamoto hiyo kusababishwa na mila na tamaduni pia mazingira yanachangia uchache huo huku akitolea mfano umbali wa viwanja katika baadhi ya maeneo.
Imeandikwa kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation