Mavunde aunda timu kushughulikia mgogoro wa naibu waziri wa zamani, wachimbaji wadogo

3 months ago 167

By  Sharon Sauwa

Mwandishi wa Habari

Mwananchi

Muktasari:

  • Serikali imepiga marufuku wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini, kuingiza wageni kutoka nje ya nchi kwenye leseni zao bila kuwa na mikataba.

Dodoma. Serikali imeunda timu ya kutatua mgogoro kati ya wachimbaji wadogo na aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, huku ikiwaondoa wageni waliokuwa wakifanya shughuli katika eneo hilo.

Mbali na hilo, Serikali imepiga marufuku wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini, kuingiza wageni kutoka nje ya nchi kwenye leseni zao bila kuwa na mikataba au makubaliano ya msaada wa kiufundi (TS) yaliyopitishwa kwa mujibu wa sheria.

Mgogoro huo unawahusisha Nkamia anayemiliki leseni ya uchimbaji mdogo na wachimbaji wadogo, uliotokea katika Kijiji cha Handali Wilaya ya  Chamwino mkoani Dodoma.

Wachimbaji wadogo wanalalamikia raia wa kigeni kuingia katika eneo lenye leseni ya uchimbaji mdogo, pia  kupigwa kwa mmoja wa wachimbaji wadogo na raia wa kigeni.

Kutokana na mgogoro huo, Julai 4, 2024, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde mbali na kutembelea eneo hilo, aliitisha kikao baina ya pande zote mbili zinazogombana.

Akizungumza leo Jumapili Julai 28, 2024, Mavunde amesema baada ya kikao kilichochukua zaidi ya saa tatu, walikubaliana kutengeneza timu itakayokwenda kupitia maduara ya wachimbaji wadogo.

Amesema lengo ni kuwezesha wachimbaji hao kulipwa fidia na kumruhusu mwenye leseni (Nkamia) kuendelea na uwekezaji huo.

Amefafanua kuwa, Serikali imezuia na kutoa katazo kwa wageni kuingia katika eneo la leseni ya uchimbaji huo.

“Nimewaambia wawaondoe wageni mara moja katika leseni ile na sasa ni shughuli ya kuyapitia maduara yote na kufahamu thamani halisi, ili waende katika hatua ya ulipaji wa fidia,” amesema.

Amesema timu hiyo iliyoshirikisha Serikali, wachimbaji wadogo na mwenye leseni, imepewa siku 28 kushughulika na jambo hilo na wanaelekea kukamilisha.

Aidha, Mavunde amepiga marufuku kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini, kuingiza wageni kutoka nje ya nchi kwenye leseni zao bila kuwa na mikataba au makubaliano ya msaada wa kiufundi yaliyopitishwa kwa mujibu wa sheria.

Pia, amepiga marufuku wageni wenye leseni kubwa za biashara ya madini, hususani wa madini ya vito kwenda machimboni kukusanya madini.

“Kufanya hivi ni kupora haki ya ajira ya Watanzania ambao kwa mujibu wa sheria, kazi ya kufuata madini machimboni inapaswa kufanywa na Watanzania pekee wenye kumiliki leseni ya ‘broker’,” amesema. 

Makusanyo yapaa

Mavunde amesema makusanyo ya wizara hiyo yameongezeka kutoka Sh677.77 bilioni mwaka 2022/23 hadi Sh822.01 bilioni mwaka 2023/24, ikiwa ni sawa na ongezeko la Sh76.08 bilioni.

Amesema ongezeko la makusanyo linalotokea kila mwaka wa fedha, linatokana na jitihada jumuishi za wadau kuanzia kwa wachimbaji, wafanyabiashara pamoja na taasisi zote zinazohusika katika kuilea na kuisimamia sekta ya madini nchini.

Kuhusu leseni ambazo hazifanyiwi kazi, Mavunde amesema wamefuta leseni 2,648 za maeneo ya uchimbaji yaliyokuwa hayafanyiwi kazi.

“Na muda si mrefu tutatengeneza utaratibu na kuutangaza kwa umma kuwa watu walio ndani na nje ya  nchi wenye nia ya kufanya uwekezaji katika sekta ya madini kutumia fursa hiyo kwa utaratibu ambao hautaturudisha kule tulipotoka,” amesema Mavunde.

Kwa upande wake, Nkamia alimpongeza Mavunde kwa kushughulikia jambo hilo kiutu uzima na kwamba timu hiyo itakamilisha kazi yake, ili waendelee na shughuli za uchimbaji kwenye eneo hilo.

“Nampongeza waziri kwa kweli amelishughulikia jambo hili kiutu uzima na tunatarajia kuwa kazi itakamilika wiki hii, ili tuendelee na kazi,” amesema Nkamia.

Source : Mwananchi

SHARE THIS POST