Kitongoji kizima cha Gaza kiliharibiwa na mikombora ya Israeli.
10 Oktoba 2024 Msaada wa Kibinadamu
Gaza mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuratibu miisaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, la afya duniani WHO na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya hatua dhidi ya mabomu UNMAS leo yamesema yamefanya jaribio la tatu kufika katika hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza, kufuatia amri ya Israel ya watu kuhama mara moja.
Wakati mashirika hayo yaikuwa yamepokea hakikisho kwamba ujumbe wao wa unaofanyika kwa hatari kubwa ungewezeshwa, vikosi vya Israeli viliwaamuru kusubiri kwa saa tano katika eneo la kusini mwa Jabalya kutokana na kukithiri kwa mapigano Jirani na eneo hilo.
Wajumbe wa operesheni hiyo ya Umoja wa Mataifa walipendekeza njia kadhaa mbadala na mbinu za kufikia hospitali hiyo, lakini hakuna iliyokubaliwa. Hatimaye, ilibidi waache operesheni hiyo na kurudi.
Misaada ya kuokoa maisha lazima iwezeshwe
OCHA imeasisitiza tena kwamba msaada wa kuokoa maisha lazima uwezeshwe huko Gaza, na hakikisho la ufikiaji salama lazima litolewe kwa uhakika. Vituo vya matibabu haipaswi kamwe kuwa uwanja wa vita na lazima vilindwe kila wakati.
Ikigeukia Ukingo wa Magharibi, OCHA imeripoti kwamba katika wiki ya kwanza ya Oktoba pekee, wanajeshi wa Israel waliwaua zaidi ya Wapalestina 20, wakiwemo watoto wanne, katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki.
Katika kipindi hiki, Wapalestina wengine 130, wakiwemo watoto wasiopungua 16 na wahudumu sita wa afya, walijeruhiwa, ama na vikosi vya Israel au walowezi wa Kiyahudi.
Jana, Mratibu Mkazi na wa Misaada ya Kibinadamu, wa Umoja wa Mataifa Gaza Muhannad Hadi, aliangazia wasiwasi unaohusiana na mavuno yajayo ya mzeituni wakati akiongoza ziara ya kidiplomasia katika kijiji cha Kifl Haris katika mkoa wa Salfit, pamoja na washirika wa kibinadamu na maendeleo.
Bwana Hadi amesisitiza kuwa mavuno ya kila mwaka ya mizeituni ni tukio muhimu la kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa Wapalestina, na kwamba mwaka jana, karibu ekari 10,000 za mashamba ya mizeituni bado hazijavunwa.
Mratibu huyo wa Misaada ya Kibinadamu ametenga dola 750,000 kutoka Mfuko wa Kibinadamu kusaidia wakulima wa mizeituni mwaka huu, akisema lazima waweze kufika bila kuzuiliwa na kwa usalama kwenye mashamba yao.
Mashambulizi dhiidi ya raia lazima yakome Gaza-UNICEF
Adele Khodr Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa UNICEF ameandika kupitia ukurasa wake wa X kwamba “Leo kumekuwa na matukio ya kutisha kutika shule ya Rufaida huko Gaza ambapo akina mama na watoto wengi waliopanga foleni katika kituo cha matibabu ya utapiamlo wameuawa na kujeruhiwa katika shambulio la anga.”
Ameongeza kuwa angalau wafanyakazi wawili wahudumu wa afya wawashirika pia waliuawa.
Khodr ametoa pole za dhati kwa familia na mpendwa wao walioathirika na shambulio la leo.
Amesisitiza kuwa “Shambulio hili linatumika kama ukumbusho mwingine wa gharama kubwa ya vita hivi inayolipwa na watoto na akina mama huko Gaza. Sio walengwa, lazima walindwe kila wakati. Mashambulizi haya dhidi ya watoto lazima yakome sasa.”