Katika tahadhari yake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR limesema kuwa mashambulizi ya awali katika wiki za hivi karibuni kando ya mpaka wa Burkina Faso na Niger tayari yamesababisha ongezeko la watu waliokimbia makazi yao katika mji wa Téra, mkoa wa Tillabéri wa Niger, licha ya hali mbaya ya kibinadamu iliyokuwepo hapo.
"Katikati ya hali ya wasiwasi wa usalama huko Tillabéri, eneo linalojulikana kwa mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali, wanaotafuta hifadhi wanaweza kukabiliwa na tuhuma zaidi za kuhusishwa na makundi haya na kuhatarisha kurejeshwa walikotoka kwa nguvu ikiwa hadhi yao kama wakimbizi haitatambuliwa na Serikali," limesema shirika hilo la UNHCR.
Shirika hilo limeendelea kusema kuwa hali hii inafuatia miaka ya ukosefu wa usalama huko Burkina Faso ambapo zaidi ya theluthi moja ya nchi inafanya kazi nje ya udhibiti wa jeshi la serikali, ambalo lilitwaa madaraka mwaka 2022.
Kwa ujumla, utulivu wa eneo la Sahel umekuwa hatarini kwa miaka mingi kutokana na ongezeo la makundi yenye silaha.
UNHCR inasema Kuanzia kaskazini mwa Mali, waasi wenye uhusiano na jihadi walishuka kusini, wakileta machafuko kaskazini mwa Burkina Faso na magharibi mwa Niger, huku pia wakitishia utulivu wa nchi nyingine jirani.
Makazi ya Tillabéri
Kwa mujibu wa UNHCR, kwa sasa,Tillabéri ni makazi ya watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi ya Niger ambao ni takriban 223,400 na waomba hifadhi kutoka Burkina Faso wapatao 36,500.
UNHCR pia inabaini kuwa mbali na wakimbizi wapya kutoka Burkina Faso, raia wa Niger wapatao 1,186 pia wamekimbia makazi yao ndani ya Tillabéri.
Kupitia taarifa yake UNCHR imesema, "Katika wiki ya mwisho ya mwezi Mei na wiki ya kwanza ya mwezi Juni 2024, makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali yalianzisha mashambulizi yakilenga raia katika majimbo ya Mansila, Kantcari na Sempelga katika Mkoa wa Sahel wa Burkina Faso".
"Ongezeko hili la mgogoro limewalazimisha waomba hifadhi wa Burkina Faso takriban 3,068 kukimbilia Téra katika mkoa wa Tillabéri wa Niger kufikia 30 Juni na hivyo kuongeza shinikizo kubwa kwa rasilimali za eneo hilo pamoja na mnepo wa jamii zinazowapokea."
Ukosefu wa usalama unaokithiri
Likibainisha hali tete ya usalama katika mpaka wa Niger na Burkina Faso, shirika la UNHCR limeeleza kuwa mashambulizi na mapigano yanaendelea kati ya wahusika wa serikali na wasio wa kiserikali na "hayawafurushi watu wengi zaidi tu, bali pia yanatatiza upatikanaji wa huduma za kibinadamu na juhudi za ulinzi".
Kama sehemu ya juhudi zake za misaada, UNHCR imekuwa ikifanya kazi na mamlaka za eneo hilo na washirika kuziandikisha mapema kaya 470 ambazo ni sawa na watu 3,068 kwa ajili ya hifadhi na kutoa msaada wa kifedha kukidhi mahitaji ya haraka.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kuwa zaidi ya watu 400 walio katika hali ngumu pia wametambuliwa kwa ajili ya msaada wa haraka, wakiwemo wanawake 207 viongozi wa kaya, wanawake wanaonyonyesha na wajawazito, na watoto wenye matatizo ya afya ya akili au walioathirika na utapiamlo.
UNHCR pia imebaini kuwa, ingawa mikakati ya kusaidia kaya 600 na makazi ya dharura na vyoo inaendelea, "kuna uhitaji wa haraka wa chakula, vifaa vya lishe, na makazi ya dharura", ikiongeza kuwa msaada wa lishe unabaki kuwa "kipaumbele, hasa kwa wale wanaosumbuliwa na utapiamlo."