Marekani yawahimiza wanawake nchini kuwa na maono makubwa

7 months ago 957

Naibu Balozi wa Marekani nchini, Robert Raines, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NAIBU Balozi wa Marekani nchini, Robert Raines, amewataka wanawake kuwa na maono makubwa ili ufadhili wanaoutoa kwa wajasiriamali uweze kuzifanya ndoto zao kuwa halisi.

Ameyasema hayo Aprili 15, 2024 jijini Dar es Salaam, wakati wa kongamano la wahitimu wa programu ya Academy for Women Entrepreneurs (AWE), iliyowakutanisha wanawake 150 kutoka mikoa tisa ya Tanzania Bara na visiwa vya Unguja na Pemba.

“Lengo la programu hii ni kuwahamasisha wanawake wawe na maono makubwa na tunawapa ujuzi wa kufanikisha ndoto hizo kubwa kuwa halisi kwa kuboresha safari zao za ujasiriamali,” alisema.
Raines amesema Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi ili kuleta matokeo endelevu.

Amesema: “Tuna furahi kuona ushirikiano wa mfuko wa Changamoto za Milenia ukirudi na zaidi ya yote namna ambavyo programu ya AWE inawainua wanawake kwa sababu tunajua ukimwezesha mwanamke, umewezesha jamii.”

“Mafanikio yako yanasisitiza kiini cha kile ambacho mpango wa AWE unalenga ambao ni kuwawezesha wajasiriamali wanawake kuwa na ndoto kubwa na kugeuza ndoto hizo kuwa mambo halisi yanayoonekana ambayo yananufaisha jamii kwa ujumla. Safari yako ya mafanikio inaangazia njia ya uvumbuzi, uthabiti na uwezeshaji wa kiuchumi,” amesema.

Raines aliongeza kuwa: Tumesisitiza mara kwa mara kwamba ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu katika Afrika ni kipaumbele cha juu cha Marekani. Tulidhihirisha dhamira hii Oktoba mwaka jana kwa kuzindua mazungumzo ya kibiashara ambayo yanaangazia sekta nne muhimu ambazo ni uchumi wa kidijitali, kuongeza ufikiaji wa soko la Marekani na Tanzania, kuboresha taratibu na mazingira ya biashara,  kuandaa misheni za kibiashara nchini Marekani na Tanzania, na kuendeleza biashara baina ya nchi zetu.” 

Amesema wanawake ambao wamepitia programu ya AWE wamekuwa ushuhuda thabiti wa moyo wa kutoshindwa, harakati zisizo na kikomo za ubora matokeo ya juhudi katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ameupongeza Ubalozi wa Marekani kwa kufadhili mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake na kwamba serikali iko tayari kushirikiana na wadau wote kukuza biashara.

“Tunafahamu nchi yetu ni uchumi wa kati kwa hivyo ukuaji wa biashara ni jambo muhimu na wanawake wajasiriamali ni sehemu muhimu katika kukuza uchumi. Wanawake wanapoimarika kiuchumi, uchumi wa familia umeimarika na wa taifa kwa ujumla.” 

Amesema: “Katika Manispaa yetu ya Kinondoni ambako mimi natokea, tuna zaidi ya Sh. bilioni 5.2 kwa ajili ya mikopo ya makundi maalum na wanawake wanayo kama Sh. bilioni mbili hivi. Wanawake waliopata mafunzo haya wana nafasi ya kupata fedha hizi,” amesema.

Mjasiriamali Magreth Masunga, kutoka Mara amesema AWE imemjengea uwezo wa kuendesha shule yake ambayo inatoa elimu ya msingi kwa mchepuko wa Kiingereza kwa gharama nafuu, ili kuwasaidia wanafunzi wanaotoka familia masikini.

“Nimepata elimu ya namna ya kusimamia biashara, ubunifu, bidii na kusimamia wafanyakazi. Leo tumejifunza namna ya kupata fedha za kukuza mitaji,” amesema.

Naye mjasiriamali Shamsa Kileo, ambaye anachakata mazao ya kilimo na kuzalisha lishe pamoja na bidhaa za urembo.

“Natengeneza bidhaa za kulinda ngozi na nywele na kwamba upande wa lishe natengeneza kwa ajili ya kupambana na njaa iliyojificha ili kukabili utapiamlo. Kwa hiyo mimi natengeneza bidhaa zenye vitamini A nyingi,” amesema.

Amesema kupitia AWE amejifunza mambo mengi ikiwamo usimamizi wa biashara, kupanga bei na namna ya kutumia muda wa biashara na familia.

AWE imeshatoa mafunzo kwa wanawake katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Dodoma, Kilimanjaro, Mara, Kagera, Mwanza, Tanga na katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Source : Kimataifa

SHARE THIS POST