Malindi haishikiki Zenji, Kibadeni apiga Hat Trick

2 months ago 16

By  Mwandishi Wetu

Mwananchi Communications Limited

MABINGWA wa zamani wa Zanzibar, Malindi imeendelea kuonyesha dhamira ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu, baada ya jana kuwanyooshaa wageni wa ligi hiyo, Inter Zanzibar kwa mabao 4-0 katika mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Annex B, mjini Unguja.

Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Malindi na kuifanya ikwee kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi sita na mabao sita kupitia michezo miwili iliyocheza hadi sasa, ikizishusha Chipukizi na KVZ ilizokuwa juu na pointi tano kila moja baada ya mechi tatu.

Katika mchezo huo, ilishuhudiwa pia hat trick ya kwanza ikifungwa msimu huu wakati straika wa Malindi, Suleiman Kibadeni Pwele, akifunga mabao matatu pekee yake, huku jingine likifungwa na mtokea benchi, Zubeir Yahya Abdul.

Kibadeni alianza kuitanguliza Malindi dakika ya 60 kabla ya kuongeza mabao mengine mawili akitumia dakika tano, akifunga la pili dakika ya 80 na lile la tatu dakika ya 85 na wakati Inter Zanzibar iliyopanda daraja msimu huu ikijiuliza, ndipo Yahya alipofunga bao la nne dakika ya 90.

Kipigo hicho ni cha pili kwa Inter Zanzibar ikizidi kujichimbia mkiani baada ya kucheza mechi mbili na zote kupoteza ikiruhusu jumla ya mabao saba na kufunga moja tu.

Katika mchezo mwingine uliopigwa kwenye Uwanja wa Annex A, Unguja, Kipanga ilijikuta ikibanwa na wageni wengine wa ligi hiyo, Junguni kwa kutoka suluhu.

Matokeo hayo yameifanya Kipanga kusalia nafasi ya nne ikiwa na pointi nne, huku Junguni ifikishe pointi mbili, huku kila timu ikicheza mechi tatu.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena jioni ya leo kwa kupigwa mchezo mmoja tu wakati New City iliyoanza msimu kwa kipigo mbele ya wageni wa ligi hiyo, Mwembe Makumbi, itakapokuwa wenyeji wa Mafunzo iliyoanza msimu na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMKM.

Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Annex A, mjini Unguja kila moja ikiwa ni mchezo wa pili kwa msimu huu, huku New City iliyopoteza kwa 1-0 kwa Mwembe Makumbi ikiwa na kazi ya kusahihisha makosa, huku Mafunzo ikitaka kuendeleza ubabe.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST