Daraja jipya la Yubu linalofadhiliwa na UNMISS ni dhabiti. Watu wengi wanaweza kusimama juu yake kwa wakati mmoja.

24 Julai 2024 Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS) umefadhili ujenzi wa madaraja matatu huko Yubu, Turbiwa na Bundri kwenye kaunti  ya Tambura jimboni Equitoria Magharibi. Lengo la ujenzi huo kupitia miradi ya matokeo ya haraka au QIPs, ni kurahisisha kurudi nyumbani kwa hiari kwa wakimbizi waliofurushwa makwao.

Madaraja hayo matatu yanalenga kuwaunganisha watu, kuimarisha mshikamano wa kijamii, na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, shule, na masoko halikadhalika utekelezaji wa jukumu la ulinzi wa raia.

Benina Mbiko, mama wa watoto watano, anaamini kwamba daraja hilo litaongeza biashara na hivyo kuinua uchumi na zaidi ya yote...

"Kwetu sisi tulio kijijini, huwa ni vigumu kuja mjini wakati wa msimu wa mvua kwa sababu maji yanapokuwa mengi, hatuwezi kuvuka mto. Daraja hili ni zuri sana, asante kwa wale waliojitokeza kutujengea."  

Kwa wengi, miundombinu mipya inayonufaisha jamii nzima ni ishara ya maendeleo yanayokuwa kama anavyoeleza Chifu Mkuu wa Kijiji cha Tambura, Mboribamo Renzi.

Anasema daraja hili litasaidia jamii kwa jumla katika nyanja za kilimo, kusafirisha bidhaa zao hadi sokoni, kurahisisha usafiri wa wagonjwa kutoka vijijini hadi mjini, kuimarisha usalama;  na haya yote ni sehemu ya maendeleo.”

Kwa upande wake, Mwakilishi wa UNMISS, Anthony Moudie, alisisitiza athari chanya za mradi kama huu akisema, ‘‘Daraja hili litasaidia au kurahisisha ulinzi wa raia wa pande zote mbili. Litasaidia serikali kupeleka vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa raia wanakuwa salama. Pia, daraja hili litafanikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa pande zote mbili.’’

UNMISS imesema itaendelea kufadhili baadhi ya  miradi midogo inayodhaniwa kuwa na uwezo wa kuboresha kwa kiasi kikubwa maisha ya jamii za maeneo ambako miradi hiyo inatekelezwa.