Laila Rashidi, mama wa watoto 10 mwenye umri wa miaka 48 kutoka jamii ya Pemba nchini Kenya akipokea cheti cha kuzaliwa kwa mwanawe. (Maktaba)
11 Oktoba 2024 Wahamiaji na Wakimbizi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetangaza kuwa zaidi ya watu nusu milioni ambao hawakuwa na uraia, wakinyimwa haki zao za kisheria, sasa wamepata uraia tangu kuanzishwa kwa kampeni ya #IBelong miaka kumi iliyopita. Kampeni hiyo, iliyolenga kumaliza tatizo la watu wasio na uraia, inakamilika mwaka huu.
Kwa mujibu wa shirika hilo kukosa uraia ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaowanyima watu haki zao za msingi kama huduma za afya, elimu, na kuwaweka katika mazingira magumu ya unyanyasaji na ukatili.
UNHCR ilizindua kampeni ya #IBelong mwezi Oktoba 2014 ili kuchochea hatua za kimataifa kumaliza tatizo hili, na mafanikio yamepatikana katika kipindi cha miaka kumi, ikiwemo kuwasaidia maelfu ya watu kupata uraia na kuboresha ulinzi kwa wale wasio na uraia.
UNHCR inasema Kampeni hii imeleta mafanikio katika nchi mbalimbali. Kwa mfano, Kenya imewapatia uraia watu wa jamii za Makonde, Shona, na Pemba, Kyrgyzstan imekuwa nchi ya kwanza duniani kutatua kesi zote zinazojulikana za ukosefu wa uraia, na Sierra Leone, Madagascar, na Liberia zimepiga hatua katika usawa wa kijinsia kwa kuruhusu wanawake kuwapatia watoto wao uraia sawa na wanaume.
Kampeni inakaribia ukingoni
Kwa sasa, UNHCR inakaribia kumaliza kampeni hii kwa kufanya mkutano wa ngazi ya juu kuhusu ukosefu wa uraia, utakaofanyika Geneva Uswisi.
Wawakilishi zaidi ya 100 wa serikali na mashirika ya kimataifa watahudhuria mkutano huo. UNHCR pia itazindua Muungano wa Kimataifa wa Kumaliza tatizo la kutokuwa na Uraia ili kuimarisha juhudi za kuhakikisha kila mtu anapata haki ya uraia bila ubaguzi.
Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR wa masuala ya ulinzi, Ruven Menikdiwela, amesema kuwa kampeni ya #IBelong imepiga hatua kubwa, lakini kazi bado haijakamilika.
"Bado kuna watu wengi ambao hawapo kwenye kumbukumbu rasmi, na wanatengwa kutokana na ubaguzi wa kikabila, kidini, au kijinsia, au kasoro katika sheria za uraia," amesema Menikdiwela.
UNHCR inaendelea kutetea haki za watu wasio na uraia na kushirikiana na washirika mbalimbali duniani ili kumaliza tatizo hili. Shirika hilo linaripoti kuwa hadi mwaka 2023, kulikua na watu milioni 4.4 wasio na uraia duniani, na takriban watu milioni 1.3 kati yao ni wakimbizi.