Afisa wa Polisi

Dakika 40 zilizopita

Immaculate Wiziri, aliyejawa na huzuni kutokana na kifo cha mpenzi wake, anahisi kutelekezwa na jeshi la polisi la Kenya ambako alijivunia kufanya kazi.

Mpenzi wake wa utotoni Jacob Masha, 32, alijitoa uhai mnamo Januari - akiwa mapumzikoni na silaha ya polisi. 

Lakini kwa vile alikufa kwa kujitoa uhai na si akiwa kazini, polisi hawajampa ushauri nasaha au msaada wowote kwa familia inayohangaika.

BBC iliomba kauli ya polisi, lakini hawakujibu.

Tangu walipopata mtoto wao wa kwanza mwaka wa 2007, wanandoa hao walikuwa wakiishi pamoja katika mji wa Malindi pwani ya Kenya.

Sawa na maelfu ya maafisa wa polisi nchini Kenya, Masha alitatizika na afya yake ya akili.

Hata hivyo hakuamini familia au marafiki kuhusu matatizo yake na shinikizo la kazi katika kikosi, ambacho alijiunga baada ya kuacha shule akiwa na umri wa miaka 18.

Maelezo ya picha,

Immaculate Wiziri anajaribu kuficha watoto wake huzuni aliyonayo.

Anakumbuka, Wiziri akimwambia mara kwa mara anahisi uchovu.

"Wakati mwingine aliniambia hali ni ngumu kazini, na kwamba hana ahata muda wa kupumzika,"anasema .

"Kwamba [kazi yake] ilikuwa ya ngumu sana, na alikuwa akifanya mfululizo. Nilikuwa nikimshauri ajipe moyo kwani sku moja utapata kitu kizuri zaidi."

Lakini huduma ya polisi ilikuwa kazi ya ndoto yake, tangu walipokutana wakiwa na miaka 15.

"Kwa muda nibaoweza kukumbuka, alikuwa akizungumzia hilo tu. Nilijivunia na kuunga mkono uamuzi wake," anasema, huku machozi yakimlenga.

Msongo wa mawazo, kiwewe na ukatili  

Inaonekana jeshi la polisi la Kenya linatambua kuwa lina tatizo - mapema mwaka huu mkuu wa polisi alisema karibu maafisa wake 2,000 walipatikana kuwa hawafai kuhudumu kwa sababu ya afya yao ya akili - kati ya jumla ya maafisa takriban 100,000.

Kulingana na takwimu za hivi punde, kulikuwa na watu 57 waliojiua mwaka jana. Kufikia sasa mwaka huu, kumekuwa na angalau mtu mmoja aliyejiua kila mwezi, na miezi kadhaa kama Aprili kuona watu kadhaa wamejiua katika wiki moja.

Data ya kabla ya mwaka  2021 haijapatikana, lakini kwa bahati mbaya tatizo hili linaonekana kukua na huenda likaeleza kwa nini polisi wamebuni jopokazi la kuboresha afya ya akili miongoni mwa maafisa.

Pamoja na kutoa vipindi vya ushauri, inataka kuhimiza utamaduni ambapo wenzako wanaweza usema nawe iwapo wanahisi kutatizika moyoni.

Demas Kiprono, msimamiz wa kampeni katika shirika la Amnesty Kenya ambaye amekuwa akitafiti afya ya akili ya polisi kwa miaka minne iliyopita, anungamkono hatua hiyo. 

"Huduma ya polisi inachukuliwa kuwa  taaluma ya ukakamavu na kuelezea hisia kunatafsiriwa kuwa udhaifu.

"Utamaduni huu umezua hali ambapo wao [maafisa polisi] wanahisi wamenaswa na inaweza kuwafanya watumie bunduki zinazotolewa na serikali dhidi yao wenyewe au kwa umma."

Kauli  hii  inaungwamkono na  mwanasaikolojia Rechael Mbugwa, ambaye amewatibu makumi ya maafisa wa polisi.

"Kwa maafisa, kutafuta msaada kunaonekana kama ishara ya udhaifu.  Watu wanawategemea wao kwa usalama kwa hivyo wanawezaje kuonekana wanyonge?

Maelezo ya picha,

Tangu utotoni, Jacob Masha amekuwa akitaka kujiunga na idara ya polisi

Mbugwa anaelezea maafisa wa polisi huwa wamekufa ganzi ili waweze kustahimili: "Aina ya kazi wanayofanya ina msongo wa mawazo na inahuzunisha sana. 

"Hali ambazo polisi wanakabiliana nazo nyingi sana - siku moja ni suala la usalama bara barani, siku nyingine ni ajali, siku inayofuata ni ghasia mara mtoto amedhulumiwa yaani wanshughulikia mambo mengi  sana."

Kiprono anaona uhusiano kati ya matatizo ya afya ya akili ndani ya jeshi na kuongezeka kwa visa vya ukatili wa polisi.

Mnamo Aprili, Amnesty Kenya ilishirikiana na Missing Voice, mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya eneo hilo, ikitoa ripoti iliyogundua ongezeko la visa vya ukatili wa polisi.

Wanaandika jinsi maafisa walivyopiga watu hadi kupoteza fahamu, kuwaibia raia na hata kuwapiga risasi na kuwaua watu wasio na hatia.

Takwimu zinashangazi:

  • 2019: Visa 145 vya mauaji ya polisi 
  • 2020: Visa 168 vya mauaji ya polisi na/au watu kutoweka
  • 2021: Visa 219 vya  mauaji ya polisi na/au watu kutoweka

"Maafisa wanapokuwa wanapokuwa na usumbufu kiakili, wataelekeza ghadhabu yao kwa umma, ndio maana tunashuhudia ongezeko la visa vya kikatili vinavyotekelezwa na polisi," anasema Kiprono.

"Kwa hivyo, ni kwa maslahi yetu kuhakikisha ustawi wa polisi [na] kuhakikisha ubinadamu wa polisi unatunzwa ili waweze kutunza usalama na haki za binadamu za watu wa Kenya."