Kitendawili Mwanachi Day! Yanga yaficha jina la timu

5 months ago 389

By  Mwandishi Wetu

Mwananchi Communications Limited

KLABU ya Yanga jana usiku ilizianika jezi mpya za msimu ujao, zilizogeuka gumzo ikiwa ni siku chache tangu watani wao, Simba kuzindua uzi wao katika hifadhi ya Mikumi, Morogoro huku mabosi wa klabu hiyo wakificha jina la timu itakayocheza nao katika Tamasha la Kilele cha Wiki ya Mwananchi, Agosti 4.

Simba ilizindua jezi na kuweka bayana tamasha lao la Simba Day linaloingia msimu wa 16 tangu lilipoasisiwa mwaka 2009, ikiitaja APR ya Rwanda iliyocheza fainali ya Kombe la Kagame 2024 na kupoteza mbele ya Red Arrows ya Zambia, lakini kwa Yanga hadi sasa imekuwa ni siri, licha ya tarehe ya tamasha kufahamika.

Yanga ambayo jana ilikuwa uwanjani kucheza na Kaizer Chiefs katika mechi maalumu ya Kombe la Toyota iliyopigwa kwenye Uwanja wa Toyota, mjini Bloemfontein Afrika Kusini hadi sasa haijaanika jina la timu itakayoshiriki tamasha la Siku ya Mwananchi itakayofanyika Kwa Mkapa, siku moja baada ya Simba Day.

“Hadi sasa jina la timu ni siri na itatolewa kama sapraizi, kama ilivyokuwa kwa jezi. Bahati nzuri tiketi za tamasha zimeanza kununuliwa na nyingine kuisha kabisa, msiwe na hofu. Bado kuna muda wa maandalizi ya tamasha na jina litaanikwa tu,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.

Msimu uliopita katika tamasha hilo, Yanga iliialika Kaizer Chief na kuifunga bao 1-0, lililowekwa kimiani na Mzambia, Kennedy Musonda ambaye bado yupo kikosini na jana alianzia benchini wakati timu hiyo ikiumana na Amakhosi kuwania Kombe la Toyota.

Yanga ilianzisha tamasha hilo mwaka 2019 ikifuata nyayo za Simba walioasisi Simba Day mwaka 2009 chini ya uongozi wa Hassan Dalali na Mwina Kaduguda na safari hii itakuwa ni msimu wa sita kwa Yanga..

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST