Muktasari:
- Mahakama hiyo imefuta sehemu ya mwenendo wa kesi hiyo kutokana na kukiuka sheria, ikiwemo mshtakiwa kupelekwa Taasisi ya akili ya Isanga.
Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imefuta sehemu ya mwenendo wa kesi ya uhujumu uchumi na amri ya Hakimu Mkazi Mkuu Dodoma, Denis Mpelembwa kwa kuwa zilikiuka sheria, hivyo mwenendo na amri hizo ni batili kisheria.
Mwenendo na amri zilizofutwa ni zile zilizotolewa Mei 21, 2024, zikihusu Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) kuwapa mkuu wa Taasisi ya Akili ya Isanga nakala za maelezo ya mashahidi. Pia, hakimu alitoa amri ya taasisi hiyo kupewa maelezo ya mshtakiwa wa pili, Olipa Mwakibete na pia mshtakiwa huyo kupelekwa katika taasisi hiyo kwa ajili ya kuchunguzwa afya ya akili.
Jaji Evaristo Longopa alitoa uamuzi huo Julai 26, 2024, ambapo alirejesha jalada la shauri hilo Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuendelea na kesi katika maeneo ambayo hayakufutwa na Mahakama hiyo kwa kukiuka sheria.
Ilivyokuwa
Katika uchambuzi wa shauri hilo, unaopatikana kwenye mtandao wa Mahakama, Mwakibete na wenzake wawili, Ashery Mwakaleja na Tulibako Angetile, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 7402 ya mwaka 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.
Wakati wa shauri hilo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ilikuwa na maoni kwamba mshtakiwa wa pili apelekwe Isanga kuchunguzwa akili kwani, alikuwa akitukana katika chumba cha Mahakama na kutoa maneno machafu ambayo hayawezi kusemwa na mtu mwenye busara au akili timamu.
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) hakuridhishwa na amri hizo na kuwasilisha maombi ya marejeo ya mwenendo wa shauri hilo na kupinga amri zilizokuwa zimetolewa.
Juni 13, 2024, DPP aliwasilisha maombi chini ya Kifungu cha 392A (1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai na kuomba Mahakama Kuu ipitie mwenendo wa kumbukumbu wa shauri hilo lililokuwa likisikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi.
Maombi
Lengo la maombi hayo lilikuwa ni kujiridhisha kuhusu usahihi na uhalali wa amri hiyo iliyopitishwa na kuhusu utaratibu wa shauri hilo na mahakama itoe amri zinazofaa kwa masilahi ya haki.
Ombi hilo liliungwa mkono na hati ya kiapo ya wakili wa Serikali, Petro Ngassa, hati ambayo ilifikishwa Mahakama Kuu Julai 25 na wakili wa Serikali Mwandamizi, Estazia Wilson.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, wakili Estazia aliomba mahakama kutengua amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mei 21, 2024, ikiitaka ofisi hiyo kuwasilisha maelezo ya mashahidi na maelezo ya mshtakiwa wa pili.
Wakili wa mshtakiwa wa pili hakupinga ombi la kufuta shauri na amri hiyo ya mahakama na kuungana na wakili Estazia kwamba amri hiyo inapaswa kufutwa.
Uchunguzi wa jaji
Jaji alieleza amesoma kumbukumbu za Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kutokana na maombi yaliyowasilishwa mbele yake ili kuthibitisha uhalali wa maombi hayo.
Upande wa mashitaka unaeleza amri hiyo ya hakimu ni kinyume cha sheria na kwa kufanya hivyo italeta madhara katika kesi.
Kumbukumbu za mahakama zinaonyesha wakati wa shauri hilo Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ilikuwa na maoni kwamba mshtakiwa hakutenda ipasavyo kama mtu mwenye akili timamu.
Kutokana na sababu hiyo, mahakama iliamua kutumia mamlaka yake chini ya Kifungu cha 220(1) na (2) ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kumpeleka mshtakiwa wa pili katika taasisi ya Isanga kwa matibabu.
Amri ya Mahakama
Amri hiyo ya mahakama ilisema mshtakiwa wa pili ameonyesha tabia zinazoashiria kwamba hana akili timamu hivyo mahakama hiyo inamweka rumande katika taasisi ya Isanga kwa ajili ya kuchunguzwa akili.
Hakimu alifikia uamuzi huo kwani mshtakiwa huyo wa pili alitukana kwenye chumba cha mahakama na kuzungumza maneno machafu ambayo hayatarajiwi kuzungumzwa na mtu mwenye busara na mwenye hali ya kawaida ya kiakili.
Mahakama iliamuru hivyo Aprili 2, 2024, lakini hakuna kilichotekelezwa na kushindwa kutekelezwa kwa amri ya mahakama ni kuidharau hivyo Mei 23, 2024, mahakama iliamuru utekelezaji wa amri hiyo ufanyike haraka.
Uchambuzi wa Jaji
Jaji alieleza kuwa uchunguzi wake wa sheria unabaini kuwa kifungu alichotumia hakimu kinaipa mahakama mamlaka ya kuahirisha shauri hilo na kuamuru mtu huyo azuiliwe katika taasisi ya akili kwa uchunguzi wa kiafya. Amesema uwezo kama huo wa mahakama unaonekana kuwa mdogo wakati wa kusikilizwa kwa kesi dhidi ya mtu kama huyo, zaidi ya hayo, kifungu hicho hakihitaji upande wa mashitaka kutoa maelezo ya mashahidi na kuwa ni maoni yake. “Agizo la kutoa maelezo ya mashahidi haliungwi mkono na sheria ambayo amri imetolewa chini yake.”
Jaji alieleza kuwa katika hatua ya mashitaka, inaonekana kuwa Mahakama inayoendesha shauri hilo haina mamlaka ya kusikiliza kifungu cha 220(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kwa vile mahakama hiyo katika hatua hiyo si inayosikiliza kesi.
Jaji alieleza utaratibu unaopaswa kufuatwa pale mshtakiwa anapokusudia kuegemea kichaa akiwa utetezi wakati wa kutenda kosa hilo ulielezwa kwa kina katika rufaa ya jinai namba 168/2025 ya MT. 81071 PTE Yusuph na wengine dhidi ya Jamhuri.
Uamuzi ulivyotoka
Maamuzi hayo yalieleza kwanza, pale inapotakiwa kutoa utetezi wa ukichaa katika shauri, unapaswa kutolewa pindi mshtakiwa anapoitwa kujibu akipandishwa kizimbani mahakama inayosikiliza kesi imeamriwa kuahirisha shauri hilo na kuamuru mshitakiwa azuiliwe katika hospitali ya magonjwa ya akili kwa uchunguzi wa afya yake.
Baada ya kupokea ripoti ya matibabu kesi inaendelea kwa njia ya kawaida huku upande wa mashitaka ukiongoza ushahidi wa kuthibitisha shitaka hilo.
Hatua nyingine ni baada ya kumalizika kesi ya mashitaka, upande wa utetezi unaongoza ushahidi kinyume na ulivyowekwa, ikiwa ni pamoja na ushahidi wa kimatibabu wa kuthibitisha ukichaa katika utendaji wa kitendo hicho.
Baada ya kuzingatia kwa kina matukio katika shauri hilo la uhujumu uchumi na amri ya Mei 21, 2024, ni maoni yangu kuwa hukumu na amri hizo ikiwemo maelezo ya mashahidi na maelezo ya mshtakiwa wa pili kupelekwa katika taasisi hiyo inakiuka sheria,” alieleza jaji.
“Hukumu na maagizo yote yametenguliwa kwa kuwa ni batili hivyo yanawekwa kando. Baada ya kutengua, jalada la awali lirejeshwe Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma kuendelea na hatua zinazohitajika kuhusu kesi dhidi ya mtuhumiwa wa pili kwa mujibu wa sheria,” alihitimisha.