Muktasari:
- Bado wachezaji walilazimika kutoroka hata msimu ulipoisha na kwenda nje kusaka malisho. Wachezaji wengi walikuwa wanatorokea Uarabuni. Ilikuwa rahisi tu kusoma katika gazeti ‘Ramadhan Lenny atorokea Uarabuni’. Ungesoma tu ‘Idd Pazi atorokea Oman’
ZAMANI tuliwahi kuishi maisha ya kushangaza sana katika soka. Mfano ni pale mchezaji anapoendelea kuwa mali ya klabu hata msimu unapoishi licha ya kutokuwa na mkataba. Zamani klabu zilikuwa hazina mikataba. Wachezaji walikuwa wanasaini katika fomu moja.
Bado wachezaji walilazimika kutoroka hata msimu ulipoisha na kwenda nje kusaka malisho. Wachezaji wengi walikuwa wanatorokea Uarabuni. Ilikuwa rahisi tu kusoma katika gazeti ‘Ramadhan Lenny atorokea Uarabuni’. Ungesoma tu ‘Idd Pazi atorokea Oman’
Wakati mwingine wachezaji walilazimika kutorokea katika viwanja vya ndege vya Zanzibar au Nairobi kwa sababu walikuwa wanahofia kuzuiwa na maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam ambao walikuwa wamejaa Usimba na Uyanga. Wao walikuwa wanawatonya mabosi wa Simba na Yanga kwamba wachezaji walikuwa mbioni kutoroka. Mara ya mwisho kusikia mchezaji kutoroka ilikuwa ni Ivo Mapunda alipokuwa Yanga alipokimbilia Ethiopia kukipiga St George. Inaelezwa Yanga ilimbania akaamua kujilipua.
Baada ya miaka mingi hatimaye, Kibu Dennis amerudia tabia hii. Maisha yamebadilika kila kitu kimebadilika lakini, Kibu ameturudisha miaka mingi nyuma. Wachezaji siku hizi wana mikataba na bado Kibu ametoroka zake kwenda Ulaya kujaribu kusaka malisho mema huko Norway. Ameenda kufanya majaribio.
Kibu ameshangaza kwa sababu mbalimbali. Kwanza kabisa hakuna nafasi ambayo wachezaji wanaililia kama kuwa mchezaji huru (free agent). Kibu alipata nafasi hii adimu. Alimaliza mkataba wake na Simba. Kwanini aliharakia kusaini mkataba mpya na Simba. Ulikuwa muda wa kutulia na kupanga hesabu zake vema.
Mchezaji mmoja wa zamani pale Ubelgiji anaitwa Jean Marc Bosman ndiye aliyewakomboa wachezaji. Zamani mchezaji angeweza kuuzwa na timu hata kama mkataba wake umeisha. Bosman alifungua kesi mahakamani na kushinda. Kwamba mchezaji akimaliza mkataba anakuwa huru. Ndio maana sheria hii inaitwa Bosman Rule.
Kuhusu Kibu, nadhani kuna watu wanajiita mameneja wa wachezaji. Hawana ‘connections’ za kuwatafutia wachezaji timu. Mara nyingi wanakuwa wepesi kusimama nyuma ya wachezaji pindi wanaposaini mkataba mpya. Hata hivyo, hawana ubavu wa kuwatafutia timu au kuwatafutia mawakala wajanja ambao wana uwezo wa kusaka timu kwa haraka.
Kibu ameleta uhuni kwa sababu ndoto yake ya kucheza Ulaya haikuanza jana wala leo. Ilianza zamani. Baada ya kumaliza mkataba wake na Simba alishapaswa kuwa na timu mikononi kwa ajili ya kusaini mkataba na klabu hizo. Na bahati nzuri kwake angeweza kupata pesa nyingi za kusaini mkataba (sign-on fee) kwa sababu alikuwa huru.
Kilichotokea ni kwamba aliamua kwa makusudi kusikiliza ofa ya Simba. Tena tuliambiwa hapa kwamba hata Yanga na Singida BS zilikuwa na ofa kwake. Kwanini aliamua kuchukua pesa ya Simba? Tena alichukua kiasi kikubwa cha pesa ambacho Simba wangeweza kukitumia kwa mchezaji mwingine katika masuala yao ya uhamisho.
Kitu kinachonishangaza ni utimamu wa akili za Kibu. Alidhani kwamba angeweza kucheza soka la kulipwa Norway bila ya kuishirikisha Simba? Iwe kwa majaribio au kusaini mkataba moja kwa moja, alidhani kwamba angeweza kusaini mkataba na wazungu bila ya Simba kuhusika? Kuna kitu kingine kinashangaza kutokana na jambo hili.
Kibu amesaini mkataba wa Simba majuzi tu. Yeye ndiye ambaye alikuwa ameshika mpini na Simba ilikuwa imeshuka makali. Kwanini asingeweka kipengele cha kuondoka kwenda kufanya majaribio au kuuzwa endapo kama kuna timu ingemuhitaji nje ya mipaka yetu. Wenzetu huwa wanalifanya jambo hilo kwa mikataba zaidi kuliko kujisumbua kutoroka.
Wakati huo huo, tunajaribu kuitazama timu ya Ulaya ambayo imempokea mchezaji wa timu nyingine bila ya kutoa taarifa. Kibu aliwadanganya kwamba ni mchezaji huru au? Hata kama aliwadanganya, lakini katika dunia ya leo ambayo kila jambo lipo mkononi, rafiki zetu wa Norway wangeutaka ukweli wangeupata mapema tu.
Na sasa wanasubiri huruma ya Simba tu katika sakata zima. Simba wakiamua kuwashtaki rafiki zao wa Norway basi nadhani rungu la FIFA linaweza kuwaangukia na wanaweza kufungiwa kwa madirisha mengi yajayo. Wameshirikiana na mchezaji husika kufanya uhuni.
Ipi nafasi ya Kibu Simba? Sijui Simba watakuwa wamesajili timu ya namna gani. Tumekuwa tukirudia kusema hapa kwamba kwa muda mrefu katika madirisha ya usajili ya hivi karibuni Simba imekosea zaidi kusajili. Labda ndio maana kuna wachezaji wanajiona muhimu zaidi na wanafanya vimbwanga.
Kama wana kikosi cha maana basi hawatakuwa wamefaya makosa kuachana na Kibu. Wanaweza kumuuza au kumtoa kwa mkopo katika timu hiyo hiyo ya Ulaya. Kama wamesajili wachezaji wa maana basi wajikumbushe tu kwamba Kibu ni mchezaji wa kawaida na kwa utovu wa nidhamu aliouonyesha basi hastahili tena kuvaa jezi ya timu yao.
Hata ukiangalia dili ambalo Simba waliweka mezani iliwashangaza wengi kwa mchezaji ambaye alikuwa ameifungia timu hiyo bao moja tu katika msimu uliopita wa Ligi Kuu. Dili lake zima kwa miaka miwili ni shilingi milioni 750 na wengi tumeguna kusikia dili hilo. Labda tu ni kwa sababu Simba waliingizwa mkenge kuwa Yanga na Singida BS wanamtaka wakahofia mashabiki wao.
Simba hawapaswi kukaa na mchezaji ambaye amejijengea taswira hii. Ilidhaniwa kwamba angeiheshimu klabu ambayo ilipambana kwa kiasi chake kumpatia uraia kama ilivyokuwa kwa Shirikisho la Soka la Tanzania. Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa yeye amewadharau. Upuuzi ulioje. Dunia ya leo unaitorokaje klabu ambayo umetoka kusaini nayo mkataba?