Jeshi la Israel limeamuru kuondoka kwa wakaazi wa vijiji 23 huko Lebanon

3 months ago 141

Jeshi la Israel limesema kuondoka huko  ni muhimu kwa usalama wa wakazi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za Hezbollah

Jeshi la Israel leo Jumamosi limewaamuru wakazi wa vijiji 23 kusini mwa Lebanon kuondoka na kwenda maeneo ya kaskazini mwa mto Awali, ambao unapita kutoka bonde la Bekaa upande wa magharibi na kuingia katika bahari ya Mediterania.

Amri hiyo iliyowasilishwa kupitia taarifa ya kijeshi, inavitaja vijiji vya kusini mwa Lebanon ambavyo hivi karibuni vimelengwa na mashambulizi ya Israel, ambapo maeneo mengi hayana watu. Jeshi la Israel limesema kuwa kuondoka huko ni muhimu kwa usalama wa wakazi, kutokana na kuongezeka kwa shughuli za Hezbollah, likidai kuwa kundi hilo linatumia maeneo kuficha silaha na kufanya mashambulizi dhidi ya Israel. Hezbollah inakanusha kuficha silaha zake kati-kati ya raia.

Mzozo kati ya Israel na Hezbollah, ulizuka mwaka mmoja uliopita, wakati kundi lililotajwa na Marekani kwamba lia kigaidi linaloungwa mkono na Iran lilipoanza kurusha roketi kaskazini mwa Israel, likiwaunga mkono Hamas mwanzoni mwa vita vya Gaza, na ulisambaa haraka ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Mashambulizi ya Israel yaliongezeka kusini mwa Lebanon, katika Bonde la Bekaa na vitongoji vya kusini mwa Beirut, yamewalazimisha takriban watu milioni 1.2 kuyakimbia makazi yao tangu Septemba 23, kulingana na serikali ya Lebanon.

Source : VOA Swahili

SHARE THIS POST